Tafuta

Hija ya Kitume ya Papa Francisko DRC na Sudan ya Kusini: Katekesi Muhtasari wa Yaliyojiri

Papa ameusia: hija ya uekumene wa haki, amani na maridhiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika lakini kwa namna ya pekee: DRC na Sudan ya Kusini. Ili kukoleza ushuhuda wa kiekumene, mshikamano na udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho, matumaini na ujenzi wa umoja wa Kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Heri Nane za Mlimani au Hotuba ya Malimani ni: Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Yeye ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo aliyedhalilishwa kwa kukamatwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo yanayopaswa kusimikwa katika utakatifu na uadilifu. Rej. Mt 5:1-12. Sehemu ya Heri za Mlimani ndiyo iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 8 Februari 2023: Kumbukumbu ya Mtakatifu Bakhita, Dada wa wote, Shuhuda wa Injili ya huduma ya upendo na matumaini ya Kikristo, Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kutembea katika utu.” Lakini kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amejikita katika ujumbe wa hija ya uekumene wa haki, amani na maridhiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika lakini kwa namna ya pekee nchi ya DRC na Sudan ya Kusini.

Papa Francisko atoa muhtasari wa hija yake ya 40 ya kitume.
Papa Francisko atoa muhtasari wa hija yake ya 40 ya kitume.

Kauli mbiu iliyonogesha hija hii kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC., kuanzia tarehe 31 Januari hadi tarehe 3 Februari 2023 ni “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Na huko Sudan ya Kusini ni “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, mshikamano na udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho, matumaini na ujenzi wa umoja wa Kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko katika hija ya 40 ya Kitume amekuwa akiambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi Dominika tarehe 5 Februari 2023 wamekuwa wakitembelea kwa pamoja Sudan ya Kusini. Huu ni shuhuda wa hija ya uekumene wa amani na matumaini kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini, kushuhudia kwamba inawezekana kwa Wakristo kushirikiana na kushikamana katika umoja na hata katika tofauti zao msingi.

Hija ya uekumene wa amani na umoja wa Kitafa
Hija ya uekumene wa amani na umoja wa Kitafa

Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kutimiza nia yake ya kutembelea DRC inayohifadhi uoto wa asili kwa ajili ya ikolojia, nchi ambayo imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa madini na maliasili nyingi, lakini, imetumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, fursa kwa wajanja wachache kufaidika na utajiri huu kwa mafao binafsi. Baba Mtakatifu akiwa nchini DRC ameguswa na amana na utajiri wa watu wa Mungu katika nchi ambayo imekuwa kama madini ya almasi ambayo yamekuwa ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko nchini DRC, kiasi cha kuwatumbukiza wananchi wa DRC katika magonjwa, umaskini na ujinga kama iliyo hata katika sehemu nyingine za Bara la Afrika. Zote hizi ni ushuhuda wa ukoloni mamboleo unaoendelea kulinyonya Bara la Afrika. Umefika wakati wa kusitisha na kuachana na mwelekeo wa unyonyaji wa rasilimali na utajiri wa Bara la Afrika. Baba Mtakatifu anasema, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa Jijini Kinshasa, kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho, ili kukoleza mchakato wa upatanisho, msamaha, ushirika na ushuhuda wa utume. Amebahatika kukutana na kusikiliza shuhuda za watu wa Mungu walioathirika kutokana na vita nchini DRC, lakini hakupata bahati kutembelea mji wa Goma ambao kimsingi ni kitovu cha athari za vita kutokana na wasiwasi wa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao. Vita na ghasia nchini DRC zinajikita katika rushwa na mafao ya watu wachache wanaotaka kujijenga kisiasa na kiuchumi.

Papa Francisko hakuweza kutembea Goma kitovu cha machafuko
Papa Francisko hakuweza kutembea Goma kitovu cha machafuko

Waathirika wa vita wamejiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu kwa kuweka silaha zao chini ya Msalaba, ili kuondokana na utamaduni wa kifo, tayari kuanza mchakato wa: imani, matumaini na upatanisho, ili kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amesema, alibahatika kukutana na kuzungumza na mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ameguswa zaidi, alipokutana na vijana wa kizazi kipya pamoja na makatekista na kuwahimiza kujikita katika maisha ya sala, ujenzi wa jumuiya inayosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; wawe ni vyombo na mashuhuda wa ukweli na uaminifu; msamaha na huduma kwa watu wa Mungu na amewaombea ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kusikiliza na kujibu kilio cha haki, amani na matumaini. Baba Mtakatifu alikazia umuhimu wa makatekista katika maisha na utume wa Kanisa ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu wanapaswa kupewa mafundisho ya: Maandiko Matakatifu, Taalimungu, Shughuli za Kichungaji, kozi ya ualimu na ufundishaji, ili hatimaye, wawe ni watangazaji mahiri wa kweli za kiimani na wawe wamejipatia mafundisho ya awali ya Katekesi.

Viongozi wa Kanisa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili
Viongozi wa Kanisa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili

Makatekista watarajiwa wawe ni wahudumu waaminifu na wanaoweza kushirikiana kwa karibu zaidi na mapadre pamoja na mashemasi, tayari kutekeleza dhamana na wajibu wao, mahali popote pale watakapotakiwa kwenda, huku wakichangamotishwa na ukweli wa hali ya kitume! Baba Mtakatifu akizungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO, alionesha moyo wa shukrani, Sura ya Kanisa linaloteseka kwa ajili ya watu wa Mungu, Msalaba wa Kristo katika maisha ya watu wa Mungu nchini DRC. Maaskofu wanahimizwa kuwa ni mashuhuda wa ukaribu wa Mungu na Unabii kwa ajili ya watu wa Mungu kwa kuunda dhamiri hai, kwa kukataa uovu na kuwatangazia watu Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu ametoa shukrani kwa viongozi wa Kanisa waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu nchini DRC na kwamba, hawana sababu ya kuogopa, bali wasimame kidete kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa furaha ya Injili, Mitume wa haki na Wasamaria wema wa mshikamano, huruma na upatanisho. Shukrani kwa wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kufanikisha hija hii ya kitume nchini DRC.

Mchakato wa upatanisho, haki na amani ni muhimu kwa maendeleo
Mchakato wa upatanisho, haki na amani ni muhimu kwa maendeleo

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia na wanadiplomasia baada ya kuwasili nchini Sudan ya Kusini, Ijumaa tarehe 3 Februari 2023 aligusia hija ya uekumene wa amani; amana, utajiri na rasilimali za nchi ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwataka viongozi kujikita katika maendeleo ya wananchi kwa kutambua kwamba, vita inaendelea kusababisha madhara makubwa. Viongozi wawe ni wahudumu na wajenzi wa amani, demokrasia, ili kupyaisha matumaini ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Vijana na wanawake wanao mchango mkubwa kwa mustakabali wa nchi yao. Ni wakati wa kujizatiti katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, kwa kujielekeza zaidi katika maendeleo fungamano ya binadamu, haki, amani na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu amesema, viongozi wa Makanisa wamefanya hija ya uekumene wa amani ili kulinda, kudumisha na kuendeleza: utu, heshima, haki msingi za binadamu, upatanisho na amani ya kudumu. Mateso, uvulivu na sadaka ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini viwalete amani ya kudumu. Hii ni nchi ambayo imebarikiwa kuwa na amana, utajiri na rasilimali nyingi na baraka ya Mto Nile, kati ya mito mirefu duniani. Utajiri wote huu, usaidie kuboresha Injili ya uhai nchini Sudan ya Kusini. Viongozi wajikite katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, wamechaguliwa na kuteuliwa ili kuwaongoza watu wa Mungu. Ni wakati wa kujizatiti katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano na kuondokana na rushwa, biashara haramu ya silaha.

Viongozi  Barani Afrika wakoleze misingi ya haki, amani na maridhiano
Viongozi Barani Afrika wakoleze misingi ya haki, amani na maridhiano

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Februari 2023 alikutana na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi kutoka Sudan ya Kusini. Katika hotuba yake aligusia matukio muhimu katika maisha ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini, dhana ya maji katika Maandiko Matakatifu; dhamana ya Musa Mtumishi wa Mungu: Unyenyekevu na Sala kama kielelezo cha wokovu wa waja wake. Viongozi wa Kanisa wajifunze Sanaa ya kutembea kati pamoja na watu wa Mungu, kutangaza na kushuhudia ukaribu wa Mungu kwa waja wake kwa njia ya sala. Viongozi wa Kanisa wawe tayari kutoka kimasomaso kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Baba Mtakatifu anasema, Sala ya Kiekumene kati ya viongozi wakuu wa Makanisa, ili kumsifu, kumtukuza na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika umoja, ushirika na utofauti wao, kushuhudia kwamba, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya uhai, upendo, haki na amani. Baba Mtakatifu katika hotuba yake alipokutana na watu wasiokuwa na makazi maalum, wakimbizi na wahamiaji alikazia umuhimu kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini na kuanza kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho; kwa kutambua na kuthamini utu, heshima na haki msingi za wasichana na wanawake ambao wana mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umoja wa Kitaifa na udugu wa kibinadamu ni muhimu kwa mustakabali wa Sudan ya Kusini.

Viongozi  Barani Afrika wakoleze misingi ya haki, amani na maridhiano
Viongozi Barani Afrika wakoleze misingi ya haki, amani na maridhiano

Baba Mtakatifu alitumia fursa hii kuwashukuru wadau wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wasiokuwa na makazi maalum, wakimbizi na wahamiaji pamoja na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa nchini humo. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amesema aligusia kiini cha hija yake ya kitume nchini Sudan ya Kusini, baada ya kuelezea sababu zinazopelekea watu wengi kuyakimbia makazi na nchi zao, amewataka watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini kujielekeza zaidi katika ujenzi wa haki na amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuwapatia watu wasiokuwa na makazi maalum fursa ya kuweza kurejea tena katika makazi yao na kuendelea kushiriki katika ujenzi wa nchi yao. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, Domika amekazia kuhusu Injili ya matumaini inayofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Amewakumbusha waamini kwamba wao ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda wa tunu hizi katika maisha na utume nchini Sudan ya Kusini, ili watu waweze kuangaziwa na: amani, wema na upendo wa Mungu, matumaini na hivyo kuendelea kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho; Ushuhuda wa Mungu ambaye ni chemchemi ya amani na faraja.

Ukarimu na upendo viwe ni vinasaba na utambulisho wa Wakristo.
Ukarimu na upendo viwe ni vinasaba na utambulisho wa Wakristo.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake Dominika tarehe 5 Februari 2023 alichambua kwa kina na mapana hekima ya Mungu ambayo imehubiriwa na Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa kuhusu Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha imani ya Kikristo na kwamba, yuko kati ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini kuwatangazia, kuwashuhudia na hatimaye, kuwaimarisha katika Injili ya matumaini, ili waweze hatimaye, kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Wageuze hali ya masikitiko katika matumaini na malalamiko yote katika furaha na kicheko. Watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini watambue kwamba, wao ni chumvi ya dunia, alama ya hekima na busara na Kristo Yesu ametumia Heri za Mlimani kuwa ni dira, mwongozo na katiba inayokoleza ladha ya utakatifu wa maisha, kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu, katika hali ya unyenyekevu, upole na huruma. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii ya Katekesi, Jumatano tarehe 8 Februari 2023 kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wakuu wa Serikali ya DRC na Sudan ya Kusini na wale wote waliojisadaka mchana na usiku kwa ajili ya kuandaa na hatimaye kukamilisha hija hii ya 40 ya Kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini kwa ufanisi mkubwa. Anawashukuru kwa moyo wa dhati kabisa viongozi wakuu wa Makanisa walioambatana katika hija ya uekumene wa amani na matumaini. Baba Mtakatifu anaiombea DRC, Sudan ya Kusini na Bara la Afrika katika ujumla wake, ili mbegu Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika upendo, haki na amani uweze kuota na kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: haki, amani,  maridhiano, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Papa DRC na S. Kusini
08 February 2023, 15:52

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >