Papa Francisko alikutana na kikundi cha vijana wa Poland wakiwa hija jijini Roma
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Kulikuwa na takriban vijana 150 na familia za mahujaji kutoka Poland ambao Baba Mtakatifu Francisko aliwapokea katika mkutano wa faragha mjini Vatican asubuhi tarehe 17 Julai 2023. Hawa ni washiriki katika mafungo, yaliyoanza Jumamosi tarehe 15 Julai, wa jumuiya ya Nuru na Uzima inayojulikana zaidi kama “Oasis of the Living Church”Yaani “Chemi chemi za Kanisa hai”, ambalo ni harakati kubwa zaidi la kikanisa nchini Poland. Kwa mujibu wa waandishi wetu wa habari Radio Vatican, wa lugha ya Kipoland Paweł Kowalski SJ na Tomasz Matyka SJ , wametaarifu kuwa Vijana na familia hizi hufuata njia ya majiundo ya Kikristo katika vikundi vyao katika parokia wakati wa mwaka na kushiriki katika kipindi kikali zaidi cha mafungo, ambacho kwa kawaida huwaleta pamoja watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Jumuiya hiyo ilianzishwa na Padre Franciszek Blachnicki, aliyeuawa mnamo mwaka 1987 na vyombo vya usalama vya kikomunisti.
Hija ya kuja Roma na kukutana na Papa ni hatua muhimu zaidi za mafungo ya ngazi ya tatu kwa vijana na familia. Washiriki walialikwa kuonja fumbo la Kanisa katika utofauti wake na lengo ni kuwasaidia kutafuta njia yao katika jumuiya ya waamini. Wanajifunza kuhusu aina na desturi mbalimbali za maombi, kushiriki katika mikutano ya kindugu na kugundua kina cha historia ya Kikristo na hali ya sasa ya Kanisa kwa kutembelea madhabahu mbalimbali.