Papa Francisko awakumbuka wahanga wa migogoro:vita ni wazimu na kushindwa
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Katekesi yake ya kwanza kwa mwaka huu 2024, akiwasalimu watu mbali waliofika katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican, tarehe 3 Januari, ametoa wito wa kuombea zawadi ya amani duniani. Kwa namna hiyo ameomba kusali kwa namna ya pekee kwa ajili ya kile kinachoendelea katika Nchi za Mashariki na katika moyo wa Ulaya. Na mwishowe wazo kwa idadi ya watu ambayo amezungumza mara kadhaa. ‘Tunawaombea watu wa Palestina, Israeli, Ukraine na maeneo mengine mengi ambapo kuna vita. Na tusiwasahau ndugu zetu wa Rohingya wanaoteswa. Tusiwasahau watu walio vitani. Vita ni wazimu. Vita siku zote ni kushindwa, daima ni kushindwa” Na tuombe kuwa na moyo nyeti kuelekea maskini na wakimbizi.
Baba Mtakatifu akitoa salamu za mahujaji wa Poland, ametoa mwaliko wa kumwomba Mwenyezi Mungu, “atujalie moyo unaojali mahitaji ya maskini, wakimbizi na wahanga wa vita. Kwa maombezi ya Maria, Mama wa Mungu, “Ninamwomba Bwana zawadi ya amani, na niwakubariki kutoka ndani ya moyo wangu!” Zaidi ya hayo, katika kutoa salamu za upendo pia kwa watakaoshiriki kipaimara na vijana wa Jimbo la Latina, aliwahimiza kutunza, kama Maria, kutafakari na kufuata Neno lililofanyika mwili huko Bethlehemu, ili kueneza miongoni mwa marafiki na wasindikizaji wao ujumbe wa heri na amani. Papa akizungumza tena kuhusu amani kwa waamini wanaozungumza Kiarabu alitoa mwaliko kwamba, na “mwanzo wa mwaka mpya, uwe wa kudumisha sala na toba ili waweze kupata ndani yake amani na furaha ambayo Mungu anataka kwa ajili yetu. Bwana awabariki wote na kuwalinda daima kutoka kwa uovu wote.”
Katika salamu zake kwa mahujaji wanaozungumza Kiingereza, Papa pia amewaombea wahanga na waokoaji wa tetemeko la ardhi huko Japan, pia akielekeza wazo kwa wale wanaofanya kazi ili kukabiliana na uharibifu na vifo vilivyosababishwa na ajali ya ndege huko jijini Tokyo nchini Japan. Idadi ya waliopoteza maisha katika tetemeko la mwaka mpya imeongezeka na kufikia watu 64, lakini hali ni mbaya mno huku mitetemeko mingine kadhaa ikiendelea kutikisa eneo hilo. Ukubwa uliorekodiwa kwa saa 4.54 za ndani ikiwa ni saa (8.54 usiku wa manane nchini Italia) katika mkoa wa Noto, katika mkoa wa Ishikawa, kwa kina cha kilomita 10 ulikuwa wa ukubwa wa 5.5. Hata hivyo hakuna maonyo ya tsunami yaliyotolewa. Japokuwa “ karibu hakuna nyumba iliyosimama. Zote zimeharibiwa kwa kiasi au kabisa,” alisema Masuhiro Izumiya, meya wa jiji la Suzu, ambalo lilipata uharibifu mkubwa.