Katekesi Kuhusu Fadhila na Mizizi ya Dhambi: Fadhila ya Haki
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kumuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua. “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Baba Mtakatifu amekwisha kuchambua mizizi hii ya dhambi hatua kwa hatua na kwamba, tiba ya uvivu ni uvumilivu wa kiimani. Amezungumzia pia kuhusu wivu, utepetevu, uchoyo, majivuno na sasa ameanza kutafakari kuhusu fadhila. Kuna fadhila kuu nne zinazotenda kazi kama bawaba ndiyo maana zinaitwa “Kuu.” Fadhila nyingine zote zajikusanya kuzizunguka nazo ni: Busara, haki, nguvu na kiasi. Kama mtu anapenda haki, basi fadhila ni matunda ya juhudi yake; kwani hufundisha kiasi na ufahamu, na haki na ushujaa. Fadhila hizi zasifiwa katika matini mbalimbali za Maandiko Matakatifu kwa majina mengine. Rej. KKK 1805. Mababa wa Kanisa wanasema, Busara ni fadhila inayoiandaa akili ya kawaida kupambanua katika mazingira yote mema yetu ya kweli na kuchagua njia zitakiwazo kuyapata. “Mtu mwenye busara huangalia sana aendavyo. Iweni na akili, mkeshe katika sala. Busara ni sheria sahihi ya utendaji ameandika Mtakatifu Thoma wa Akwino, akimfuata Aristotle. Busara isichanganwe na hofu au woga, wala hila au udanganyifu. Hekima huitwa “Auriga virtutum” yaani “Mwendesha fadhila; huongoza fadhila nyingine kwa kuweka sheria na kipimo. Ni busara inayoongoza mara moja hukumu ya dhamiri. Mtu mwenye busara huamua na kuongoza mwenendo wake kulingana na hukumu hiyo. Kwa msaada wa fadhila hii tunatumia misingi ya maadili katika masuala ya pekee bila kosa na kushinda mashaka ya mema ya kupata, na mabaya ya kuepuka. Rej. KKK. 1806. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia pia fadhila ya subira katika maisha na utume wa Kristo Yesu.
Haki ni fadhila ya kibinadamu na Mababa wa Kanisa wanasema, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. Haki kwa Mungu huitwa “Fadhila ya Kimungu.” Haki kwa watu yaelekeza kuheshimu haki za kila mmoja, huanzisha mapatano katika mahusiano ya kibinadamu yanayoendeleza usawa kuhusu watu, mali ya Jumuiya. Mtu mwenye haki, anayetajwa mara nyingi katika Maandiko Matakatifu hutofautishwa kwa kawaida ya mawazo yake, unyofu wa mwenendo wake kwa jamii. “Usimpendelee mtu maskini, wala kumstaajabia mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki na adili, mkijua kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni.” KKK 1807. Fadhila ya haki inajulikana pia kwa lugha ya Kilatini kama “Unicuique suum.” Hii ni sehemu ya Katekesi kuhusu fadhila ya haki iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Aprili 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu kuhusu fadhila ya haki, amekazia kuhusu fadhila mbadala zinazowawezesha watu kuishi kwa amani, mtu wa haki daima yuko tayari kuomba msamaha, ni shuhuda wa kanuni maadili na utu wema, kwa hakika watu wa haki ni wachache sana ndani ya jamii, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa ni watu wa haki. Katika maisha ya jamii, kila mtu anapaswa kutendewa kwa haki sanjari na kuheshimu utu wake wake. Fadhila ya haki inadai fadhila nyingine kama: ukarimu, heshima, shukrani, urafiki, uaminifu na kwamba hizi fadhila zinazochangia kuishi pamoja kwa watu vizuri.
Bila haki anasema Baba Mtakatifu hakuna amani na kwamba, sheria ambayo ingetawala ni ile ya “Mwenye nguvu mpishe.” Haki inapaswa kutekelezwa kwenye vyombo vya sheria, lakini pia inapaswa kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha ya kawaida katika ukweli wote na haki. Mtu wa haki anaonekana hata katika kuzungumza kwake, daima ni kielelezo cha moyo wa shukrani na ukarimu na anatambua kwamba, yeye amependwa kwanza. Mtu mwenye haki huheshimu na kutii sheria; ni mtu anayejikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mtu mwenye haki anapenda kuratibu maisha yake, anapokosea yuko tayari kuomba msamaha; ni mtu anayewajibika pamoja na kuheshimu sheria za nchi; ni mtu asiyependa kutoa wala kupokea rushwa; anaridhika na kipato cha maisha yake. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kujikita katika utawala wa sheria bila shuruti, dawa mchunguti katika kudhibiti rushwa na ushuhuda wa uwongo. Zaidi ya hayo, mtu wa haki na mwadilifu huepuka tabia mbaya kama vile: kashfa, ushuhuda wa uongo, ulaghai, riba kubwa, dhihaka na ukosefu wa uaminifu. Mwenye haki hushika neno lake, anarudisha alichokopa, anatambua mshahara sahihi kwa wafanyakazi wote: mtu asiyetambua mshahara sahihi kwa wafanyakazi si mwadilifu, ni dhalimu. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, ulimwenguni humu kuna watu wachache sana wenye haki. Kimsingi hawa ni watu wanaovuta neema na baraka; ni watu wanaoheshimika na kupendwa. Watu wenye haki na wadilifu wanao kiu ya haki, watu wa ndoto wanaohifadhi katika sakafu ya nyoyo zao, shahuku ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Kimsingi, walimwengu wanawahitaji watu wa haki, watakaowashirikisha wengine furaha ya kweli.