Papa Francisko atuma dawa za dharura nchini Ukraine
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika moyo wa Papa Francisko daima kumekuwa na kuteswa kwa nchi ya Ukraine, ambayo anaelekeza mawazo yake kila mara huku akitualika kusali kwa ajili ya amani. Tangu mwanzo wa vita kumekuwa na ishara nyingi za ukaribu na mshikamano: kama vile kuanzia na ununuzi wa jenereta hadi kupeleka chakula, nguo za joto na mablanketi. Kufuatia kile kilichofanyika siku za nyuma, mnamo Jumamosi iliyopita tarehe Mosi Juni 2024, Papa Francisko alituma dawa za huduma ya kwanza nchini humo, hasa zilizokusudiwa kwa ajili ya majeruhi wa vita, zenye thamani ya euro laki moja, ambapo ni matokeo ya mchango muhimu uliopokelewa na Shirika la Misaada ya Kitume kwa njia ya Ubalozi wa Vatican.
Hii ni njia ya kuwa karibu na watu katika shida kubwa, iliyojaribiwa na zaidi ya miaka miwili ya migogoro. Tahadhari kwa wale walio pembezoni ni utume ambao Papa amewakabidhi kwa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Huduma ya Upendo hivyo, katika Juma hili kuna pia huduma ya upimaji wa afya iliyoanzishwa mjini Vatican kwa wale ambao wanahitaji msaada huo. Hawa ni karibu watu 50 ambao hawawezi kufikia Mfumo wa Kitaifa wa Afya Italia na ambao, mara nyingi, hawajui kuwa wanaweza kuwa hatarini kwao wenyewe na kwa wengine.
Kuzuia saratani ya matiti
Msisitizo pia ni kuzuia, hasa wanawake wanaoishi pembezoni, bila huduma ya afya na kwa kawaida hufuatwa na kliniki ya “Madre di Misericordia yaani Mama wa Huruma ” na Zahanati ya Mtakatifu Marta. Mnamo tarehe 18 Aprili iliyopita, gari kutoka Komen Italia, ya Chama kinachojishughulisha na kinga na mapambano dhidi ya saratani ya matiti, ambacho kimekuwa katika harambee kila mara na Taasisi ya Mfuko wa Hospitali ya Agostino Gemelli (IRCCS) na Kisiwa cha Gemelli Tiberina kimewapa takribani wanawake arobaini maskini fursa ya kunufaika na vipimo vya uchunguzi kwa ajili ya kujikinga na saratani ya matiti kwa kutumia vipimo vya ultrasound ya matiti. Uzoefu huo, ambao hudumu kila baada ya miezi miwili, pia unaarudiwa mwezi huu Juni. Kwa upande wa Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo amebainisha kuwa, “mipango inayotekelezwa ni ishara ya Injili inayokaribia, inayowaangalia wale wanaoteseka bila kuangalia upande mwingine.”