Tafuta

Papa ametoa wito tena wa kusitisha silaha na ghasia. Papa ametoa wito tena wa kusitisha silaha na ghasia.  (REUTERS)

Papa Francisko,Mashariki ya Kati:kusitisha mapigano katika nyanja zote

Mwishoni mwa Katekesi,Papa alizindua wito mpya ili mzozo kati ya Israeli na Hamas usienee na kuomba silaha zisitishwe kuanzia Gaza,ambapo hali ya kibinadamu sio nzuri.Upendo ushinde chuki na kulipiza kisasi,Silaha ziondolewe kwa msamaha.Hakusahau kuombea nchi ya Ukraine inayoteswa,Myanmar,Sudan,Pakistan na Afghanistan ili ubaguzi ukomeshwe dhidi ya wanawake.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi iliyonza tena mara baada ya mapumziko ya mwezi Julai, Jumatano tarehe 7 Agosti 2024 hakuweza kuficha wasiwasi wake kuhusu hali ya Mashariki ya Kati. Wakati hofu inaongezeka juu ya uwezekano wa shambulio la Iran kwa Israeli na mvutano na Lebanon ukiendelea, Papa Francisko kwa mara nyingine tena aliomba uhasama usitishwe. Haya yamesikika wakati akitoa salamu kwa lugha ya Kiitaliano kwa mahujaji waliokusanyika katika Ukumbi wa Paul VI mjini Vatican.

“Narudia wito wangu kwa pande zote zinazohusika ili mzozo usienee na kwamba moto ukome mara moja katika pande zote, kuanzia Gaza, ambapo hali ya kibinadamu ni mbaya sana na haiwezi kudumu.”

Upendo utawale

Matumaini ya Papa Francisko ni kwamba upendo unashinda na kwamba uhasama unatatuliwa kwa msamaha. “Ninaomba kwamba utafutaji wa dhati wa amani uzime mabishano, upendo ushinde chuki na kisasi kiondolewe kwa msamaha.”

Kuwe na amani katika Ukraine, Myanmar na Sudan

Baba Mtakatifu Francisko pia alionesha wasiwasi wake kwa Ukraine na kuwaalika waamini kuiombea nchi ya Ulaya Mashariki na mataifa yaliyo katika vita ambapo watu wanaendelea kuteseka na matatizo na maumivu makali.

“Ninawaomba muungane na katika maombi yangu kwa ajili ya Ukraine inayoteswa, Myanmar na Sudan. Wacha watu hawa, waliojaribiwa sana na vita  wapate amani inayotamaniwa haraka iwezekanavyo.”

Kuondoa ubaguzi nchini Pakistan na Afghanistan

Hatimaye, Papa  Francisko  ambaye kabla ya Katekesi alikutana na uwakilishi kutoka chama cha  Jumuiya ya Afghanistan nchini Italia aliomba, pia Pakistan na Afghanistan ambapo wengi bado wanabaguliwa.

“Tuunganishe juhudi na maombi yetu ili kuondoa ubaguzi wa kikabila katika mikoa ya Pakistan na Afghanistan, hasa ubaguzi dhidi ya wanawake.”

Mara baada ya Katekesi Papa ametoa wito wa kusitisha vita
07 August 2024, 16:03