Katekesi Kuhusu Roho Mtakatifu na Bibi Arusi: Roho Mtakatifu na Shetani, Ibilisi

Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 25 Septemba 2024 imejikita kwa Roho Mtakatifu aliyemwongoza Kristo Yesu Jangwani na kwamba, Roho Mtakatifu ni mwenza wa waamini katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi. Mwenyezi Mungu ndiye aliyemtuma Kristo Yesu kwenda Jangwani na baada ya kushinda majaribu yote ya Shetani, Ibilisi “Yesu akarudi kwa nguvu za Roho Mtakatifu.” Lk 4:14. Ma Modesta Kaigalura kutoka Bukoba, Tanzania ametia neno!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafumbo ya maisha ya Yesu ya hadhara yanafumbatwa katika Ubatizo mwanzo wa maisha na utume wake kama Mtumishi anayeteseka, Mwana kondoo wa Mungu anayechukua dhambi ya ulimwengu, tayari kutimiza mapenzi ya Baba wake wa mbinguni. Kristo Yesu alisukumwa na Roho Mtakatifu Jangwani, Kristo Yesu alibaki siku arobaini akifunga na kusali. Baada ya kumaliza siku hizo, Shetani alimjaribu mara tatu akitafuta kuupima msimamo wake wa kuwa ni Mwana wa Mungu. Kristo Yesu anashinda majaribu yote haya na Ibilisi anajitenga naye tayari kurudi kwake kwa wakati. Kristo Yesu anajifunua kama Mtumishi wa Mungu aliye mtii na mshindi dhidi ya Ibilisi. Huu ni ushindi wa mateso, na wa utii mkubwa wa Mwana wa Baba wa milele. Rej. KKK 535-540. Roho Mtakatifu ni mdau mkubwa wa waamini katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi na mambo yake! Rej. Lk 4:1-2. 13-14. “Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na Malaika walikuwa wakimhudumia.” Mk 1:12-13. Baba Mtakatifu Francisko anasema jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua kuwa “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Huu ni muda uliokubalika wa kuingia katika jangwa la maisha ya kiroho, yaani upweke, ili kusikiliza kile kinachotoka moyoni, ili hatimaye kukutana na ukweli wa maisha.

Umati wa waamini uliofurika kwenye Katekesi ya Papa Francisko
Umati wa waamini uliofurika kwenye Katekesi ya Papa Francisko

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo, Jumatano tarehe 29 Mei 2024 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu.” Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 25 Septemba 2024 imejikita kwa Roho Mtakatifu aliyemwongoza Kristo Yesu Jangwani na kwamba, Roho Mtakatifu ni mwenza wa waamini katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi. Mwenyezi Mungu ndiye aliyemtuma Kristo Yesu kwenda Jangwani na baada ya kushinda majaribu yote ya Shetani, Ibilisi “Yesu akarudi kwa nguvu za Roho Mtakatifu.” Lk 4:14. Kristo Yesu akarudi akiwa ni mshindi, tayari kuwakomboa wale wote wanaoteswa kwa nguvu za Shetani, Ibilisi, kielelezo cha uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya waja wake. Shetani, Ibilisi yupo na anaishi na kwamba, dunia imesheheni matendo ya Shetani, Ibilisi, licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Baba Mtakatifu anasema, ukimshinda Shetani, Ibilisi kwa imani, anaingia kwa mkwara wa uchawi. Ikumbukwe kwamba, Shetani, Ibilisi anaishi si tu na wadhambi, bali hata na watakatifu wateule wa Mungu; anaishi katika matendo maovu ambayo mwanadamu anakutana nayo kila siku ya maisha yake!

Roho Mtakatifu ni mdau katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi
Roho Mtakatifu ni mdau katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi

Si rahisi kumtambua Shetani, Ibilisi anapotenda kazi yake, ndiyo maana Mama Kanisa anatumia hekima na busara anapowinga na kupunga pepo. “Exorcizare, Exorcism.” Hekima hii ya Kikristo ni ustawi unaothibitisha kabisa hadhi ya kila mtu kama mwana wa Mungu, huanzisha udugu wa msingi, hufundisha kukabiliana na maumbile, kama kufanya kazi na hutoa sababu za kuishi kwa furaha na utulivu katikati ya ugumu wa maisha. Hekima hii pia kwa ajili ya Taifa ni msingizi wa upambanuzi na msukumo wa Kiinjili unaolifanya kuonja mara moja wakati Injili inapohudumiwa katika Kanisa na wakati yaliyomo yanatupwa nje na kusongwa na mambo mengine. Rej. KKK 1676. Kumbe, waamini watakatifu wa Mungu wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumtambua Shetani, Ibilisi katika maisha yao, tayari kumfukuzia mbali kwa mwanga wa Injili. Baba Mtakatifu anatoa angalisho kwa waamini kamwe wasithubutu kujadiliana na Shetani, Ibilisi, wawe macho na wakeshe na kamwe wasimpatie nafasi hata kidogo katika maisha yao. Rej. Efe 4:27 na 1Pet 5:8. Kristo Yesu alimshinda Shetani, Ibilisi kwa njia ya Msalaba. Shetani, Ibilisi anashawishi kwa kutumia Amri za Mungu na kwamba, anatumia njia na nyenzo nyingi kuweza kuwanasa watu na kuwateka katika himaya yake. Mawazo ya uwepo wa Shetani, Ibilisi katika historia, iwe ni chemchemi ya imani na usalama, kwani Kristo Yesu ameshinda nguvu za Shetani, Ibilisi na amewakirimia waja wake Roho Mtakatifu, ili awajalie ushindi kwa njia ya utakaso wa dhambi, ili hatimaye, aweze kuwakirimia amani na kuwaepusha matendo ya giza, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Ma Modesta Kaigalura katika ubora wake Radio Vatican.
Ma Modesta Kaigalura katika ubora wake Radio Vatican.

Mama Modesta Kaigalura kutoka Tanzania ni kati ya waamini walioshiriki katika Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 25 Septemba 2024 mjini Vatican. Mama Modesta anasema, anatoka Parokia ya Buyango, Kigango cha Kabashana, hiki ni Kijiji maarufu sana Jimbo Katoliki la Bukoba, lakini kwa miaka mingi wameishi Parokia ya Mtakatifu Francisko Xsaveri, Jimbo kuu la Dar es Salaam, anazungumzia furaha yake kuu ya kushiriki katika Katekesi ya Baba Mtakatifu, Sala na maombezi kwa familia yake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na umuhimu wa wazazi na walezi kukuza mbegu ya miito mitakatifu katika watoto wao! Yaani, Ma Modesta Kaigalura, leo alikuwa na furaha ya ajabu, lakini amemkumbuka Ta… ambaye amebaki “home” akiangalia familia.

Katekesi Roho Mtakatifu
25 September 2024, 15:14

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >