Ukaribu wa Papa kwa Kard.Parolin kufuatia na kifo cha mama yake Ada
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, katika telegram yake kwa Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, anaelezea kujulishwa kifo cha mama yake mpendwa, Bi Ada, kilichotokea Jumamosi tarehe 31 Agosti 2024, na kwa hiyo anashiriki kiroho katika maombolezo ambayo yameikumba familia hiyo huku "ahakikishia ukaribu wake katika wakati huu maalum wa mateso ya mwanadamu." Papa ameongeza kuandika kuwa: “Nikimkabidhi ndugu yetu mpendwa kwa huruma ya Baba atoaye uzima ninainua sala yangu kwa Bwana ili amkaribishe katika furaha ya milele na kwa wanafamilia wote mnaoomboleza kifo chake ninawaombea faraja katika imani katika Kristo mfufuka na kwa moyo wote ninatuma baraka zangu za kibaba.”
Mazishi ya Bi Ada Miotti Parolin, aliyefariki dunia kwa amani akiwa na umri wa miaka 96, yaliogozwa na mwanae, Kardinali Parolin, Jumanne tarehe 3 Septemba 2024, saa 3.30 asubuhi katika Kanisa la Parokia ya Schiavon, jimbo la Vicenza nchini Italia. “Asante mama, kwa magoti yako tulijifunza kuhusu Injili,” alisema Kardinali Parolin katika mahubiri ya misa hiyo, huku sauti ikisikika na hisia kali na kusisitiza kuwa: “leo imani hiyo katika ufufuko tunao amini umetimizwa kwa mama." Kwa kuongezea akiwageukia waamini katika misa hiyo alisema: "Ninyi ambao sasa mnatuona hapa tunafurahi na kushukuru kwa ushiriki wenu mkubwa.” Kwa njia hiyo mara baada ya misa ya mazishi mwili wake ulilazwa kwenye makaburi ya Schiavon. Wakati Mkesha wa maombi kwa ajili ya marehemu huyom ulifanyika Jumatatu tarehe 2 Septemba2024, saa 1.30 jioni, katika Kanisa hilo la Schiavon.