Katekesi Kuhusu Roho Mtakatifu na Bi Arusi: Roho Mtakatifu na Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo, Jumatano tarehe 29 Mei 2024 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu.” Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 25 Septemba 2024 ilijikita kwa Roho Mtakatifu aliyemwongoza Kristo Yesu jangwani na kwamba, Roho Mtakatifu ni mwenza wa waamini katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi. Mwenyezi Mungu ndiye aliyemtuma Kristo Yesu kwenda Jangwani na baada ya kushinda majaribu yote ya Shetani, Ibilisi “Yesu akarudi kwa nguvu za Roho Mtakatifu.” Lk 4:14. Kristo Yesu akarudi akiwa ni mshindi, tayari kuwakomboa wale wote wanaoteswa kwa nguvu za Shetani, Ibilisi, kielelezo cha uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya waja wake. Shetani, Ibilisi yupo na anaishi na kwamba, dunia imesheheni matendo ya Shetani, Ibilisi, licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.
Baba Mtakatifu anasema, ukimshinda Shetani, Ibilisi kwa imani, anaingia kwa mkwara wa uchawi. Ikumbukwe kwamba, Shetani, Ibilisi anaishi si tu na wadhambi, bali hata na watakatifu wateule wa Mungu; anaishi katika matendo maovu ambayo mwanadamu anakutana nayo kila siku ya maisha yake! Mababa wa Kanisa wanasema, Kanisa, ushirika hai katika imani ya Mitume ambayo linaiendeleza, ni mahali muafaka pa kuweza kumfahamu Roho Mtakatifu: Katika Maandiko Matakatifu ambayo ameyavuvia; katika Mapokeo ya Kanisa yanayoshuhudiwa na Mababa wa Kanisa; Katika Mamlaka ya ufundishaji katika Kanisa “Magisterium” ambayo anayauauni, Katika Liturujia ya Sakramenti kwa njia ya maneno na alama zake, ambazo Roho Mtakatifu huwaingiza waamini katika ushirika na Kristo Yesu; Katika Sala ambamo anawaombea waamini; Katika karama na huduma zinazolijenga Kanisa; Katika ishara za maisha ya kitume na kimisionari; Katika ushuhuda wa watakatifu, ambamo anadhihirisha utakatifu wake na anaendeleza kazi ya wokovu. Roho Mtakatifu na Kanisa: Utume wa Kristo Yesu na wa Roho Mtakatifu unakamilika katika Kanisa, mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hutayarisha watu, akiwaendea kwa neema yake ili kuwapeleka kwa Kristo Yesu. Anamdhihirisha kwao, analifanya Fumbo la Kristo liwepo kwao na mwisho huwapatanisha na kuwaweka katika umoja na Mwenyezi Mungu, ili wazae matunda mengi. Kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Kristo Yesu anavishirikisha viungo vya mwili wake Roho wake Mtakatifu na Mtakasaji. Kumbe, Kanisa ni Sakramenti ya umoja wa Fumbo la Utatu na wa watu. Rej. KKK 683-747.
Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 9 Oktoba 2024 ameendeleza Katekesi kuhusu Roho Mtakatifu na Kanisa mintarafu Matendo ya Mitume, Siku ile ya Pentekoste ya kwanza, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kwa kasi; kukatokea ndimi zilizogawanyika, kama ndimi za moto na wakaanza kuzungumza kwa lugha nyingine. Roho Mtakatifu ndiye anayelihakikishia Kanisa umoja, baada ya kumpokea Roho Mtakatifu, Mitume walianza kuzungumza kwa lugha na kutoka nje kwenda kumtangaza na kumshuhudia, kielelezo cha utume wa Mama Kanisa katika kutangaza na kushuhudia hadi miisho ya dunia; katika toba na wongofu wa ndani kama ilivyotokea kwa Akida Kornelio kule Kaisaria, na hiyo ikawa ni Pentekoste mpya, iliyobomoa ukuta wa utengano kati ya Wayahudi na Wapagani, waliomwongokea Kristo Yesu katika maisha yao na Kanisa likakua na kupanuka kijiografia, utume uliofanywa na Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kwa maongozi ya Roho Mtakatifu. Rej. Mdo 16:6-10. Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa pia Bithinia hadi wakafika Makedonia na huko wakahubiri Habari Njema ya Wokovu.
Roho Mtakatifu ndiye anayeunda umoja wa Kanisa kama ilivyotokea katika mabishano huko Antiokia juu ya tohara kama Mtume Paulo anavyoandika kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, Sura ya 15. Kuhusu utatuzi wa mabishano hayo, uliofikiwa kwa kuitisha Mtaguso mkuu wa kwanza wa Yerusalemu, hapa umoja wa Kanisa ukapatikana tena baada ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi na Waraka wa Mtaguso mkuu wa Yerusalemu unahitimishwa kwa kusema, “Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima.” Mdo 15:28. Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, Roho Mtakatifu anatenda kwa ajili ya Fumbo la Mwili wa Kristo ambalo ni Kanisa na anatenda kazi zake kutoka katika undani wa Kanisa ili kuimarisha kifungo cha umoja na kwamba, Roho Mtakatifu mwenyewe ndiye kifungo cha Umoja: “vinculum unitatis.”
Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba waamini wengi wanapenda umoja wa Kanisa kutoka katika “sakafu za nyoyo zao”, lakini umoja ni changamoto pevu kama inavyojionesha kwenye Sakramenti ya ndoa na maisha ya kifamilia; Umoja, upendo, mshikamano na maridhiano ni kati ya changamoto mamboleo katika maisha ya mwanadamu, si rahisi kuweza kufikiwa sembuse kuendelezwa. Hii ni changamoto ya kufikiri na kutenda katika ujenzi wa umoja kama ulivyoasisiwa wakati wa Sherehe ya Pentekoste ya kwanza mintarafu Roho Mtakatifu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu. Hata ujenzi wa umoja wa Wakristo unapaswa kuwahamasisha Wakristo ili waweze kutembea kwa pamoja katika umoja, ili kumwendea Kristo Yesu. Hii ni changamoto kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya umoja na amani.