Hospitali ya Bambino Gesu’:Papa awabembeleza watoto wa Ukraine!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 19 Machi 2022 katika siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, mida ya saa 10.00 za jioni hivi alikwenda katika Hospitali ya watoto ya Bambino Gesù ili kuwatembelea watoto waliolazwa kutoka Ukraine, kwa siku za hivi karibuni tangu kuanza vita. Baba Mtakatifu Francisko alipokelewa na Rais wa Hospitali hiyo Bi Mariella Enoc, ambaye alimsindikiza katika Wadi mbali mbali za Hospitali ya Watoto.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Vyombo vya habari Vatican, Dr. Matteo Bruni kwa waandishi wa habari alisema kuwa kwa sasa ni watoto 19 kutoka ukraine walio katika hali ngumu na ambao wako kwenye vituo mbali mbali jijini Roma kuanzia Gianicolo na Palidoro, kilomita chache kutoka mji mkuu, vikiwa ni sehemu ya Hospitali ya Watoto Bambino Gesu.
Waliofika mwanzoni mwa vita kutoka Ukraine walikuwa karibu watoto 50 wenye magonjwa mbalimbali kama saratani, magojwa na akili na aina nyingine za magonjwa ambao walikimbizwa mara moja baada ya kuanza kwa vita. Wengine wana majeraha makubwa. Papa Francisko alikwenda kwenye vitanda vyao na kuwatembelea wadogo hao kabla ya kurudi mjini Vatican.