Ukraine,Kard.Parolin:Diplomasia haijapata ufanisi mkubwa
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Alhamisi tarehe 24 Novemba 2022, Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican akizungumza nje ya uzinduzi wa Mwaka wa masomo 2022-2023, katika Chuo Kikuu cha Ulaya, Roma Italia, akihojiwa na mwandishi wa Televisheni ya Baraza la Maaskofu Italia (TV 2000), kuhusiana na suala la vita nchini Ukraine, alisema kwamba “mchakato wa diplomasia katika vita nchini Ukraina hadi wakati huu haukuleta matokeo makubwa”. Kwa mujibu wake alisema hiyo “inategemea na sehemu zote mbili”.
Uwezekano wa kuingilia kati katika kutaka amani kwa upande wa Vatican “umekuwapo tangu mwanzo wa vita. Papa mara kadhaa amekuwa akirudia kuonesha utashi huu wa kusitisha vita, lakini hata utayari wa kutoa msaada wa hali na mali katika muktdha huo ili kuweza kufikia mwisho wa vita hivyo. Hadi sasa lakini hapajaonekana jibu” alisisitiza.
Kwa hiyo alisema kwamba kuna sehemu tatu ambazo Vatican imekuwa ikijikita nayo kwa mujibu wa maelezo ya Kardinali Parolin: Kwanza kabisa ni majisterio ya Papa katika miito yake isiyositishwa kwa ajili ya kumaliza vita hivyo; pili kuna muktadha wa ubinadamu ambao amekuwa akisisitiza kwa sababu hali ya Ukraine inaendelea kuwa ngumu zaidi kwa watu ambao hata sasa wameachwa katika giza na baridi kwa sababu ya kulipuliwa vituo vya umeme na huduma vya kiraia, jambo ambalo kweli ni muhimu sana; na tatu kuna matendo hai ya kidiplomasia ambayo hadi sasa hayajazalisha matokeo makubwa.