Papa kwa Caritas Jimbo la Toledo:muwe stadi wa hekima inayohitajika sana ulimwenguni!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko alikutana mjini Vatican, tarehe 5 Desemba 2024 na takriban washiriki mia moja wa Caritas Jimbo la Toledo, nchini Hispania, katika Ukumbi wa Uchaguzi mjini Vatican. Tukio la mkutano wao ni katika kumbukizi ya miaka 60 ya shirika la kutoa misaada, lililoanzishwa mnamo tarehe 2 Juni 1964. Katika hotuba yake aliwakaribisha na kuungana nao katika shukrani zao kwa miaka sitini ya huduma ya upendo katika Kanisa la Toledo. Ahadi ambayo, kama alivyoweza kusisitiza kwamba inakwenda mbali zaidi ya mema madhubuti yanayoweza kufanywa kwa mtu, kukubali changamoto ya kuwa kichochezi cha mabadiliko katika jamii kwa kueneza moyo wa upendo na haki, ili kuamsha dhamiri ya kidugu zaidi kwa watu wote wenye mapenzi mema. “Yaani udugu wetu wakati fulani unalala au haukui. Na dhamiri ya kidugu inapochochewa ni kuiamsha tena na kuifanya ikue."
Kwa kufanya hivyo, Papa aliongeza, wao wanakuwa siyo kielelezo cha ustaarabu tu na uhisani, bali pia wanakuwa vyombo vya uinjilishaji, kupitia lugha ya ulimwengu ya kazi za upendo. "Inashangaza, kazi za upendo mara kadhaa hazihitaji mfasiri, hakuna kamusi ya kutafsiri, lugha ya ulimwengu wote, lugha ya ulimwengu ya kazi za upendo kila mtu anaielewa." Kwa sababu hiyo ni lugha inayoeleweka kwa wote, iliyoandikwa kwa ushuhuda na juhudi za mawakala wote wa Caritas, waliokabidhiwa kwa Yesu Kristo na Injili yake, Papa Francisko alisisitiza. Ni lengo la juu bila shaka, ambalo linafikiwa kupitia kazi ya ufundi ya kila mmoja wa wale wanaohusika na hatua ya usaidizi wa kijamii, kuanzia malezi ya kibinadamu na ya kiroho ambayo inawaruhusu kushughulikia kwa uthabiti shida za kijamii zinazobadilika kila wakati, kwa kuzingatia hali ya kijamii na mafundisho ya Kanisa. Bila kusahau moyo wa ushirikiano na sinodi pamoja na ukweli mwingi wa kichungaji unaounda Kanisa zima la kijimbo.
Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Francisko aliwatia moyo wasonge mbele katika juhudi hiyo, wakijifunza daima, kutoka kwa Bwana, katika kitabu hai cha sala na usomaji wa Neno lake, katika kitabu hai cha uzoefu wa sakramenti na kusikiliza kwa makini sauti ya wachungaji wake na kwa uwepo wake katika Ekaristi na katika wale wanaowahudumia. Baba Mtakatifu kwa kuhitimisha alisema: “Kitu kimoja ninachowaomba ni kwamba muwe walimu wa hekima, wa hekima hiyo ambayo ulimwengu unahitaji sana. Ujinga unashangaza. Unauza na kununua ujinga, na bei sio ofa, ya kufilisi, ni bei za msimu, bei ghali. Na tafadhali, nawaomba mniombee. Kwa Yesu, ambaye kwa kila mtu hasiye na pa kulaza kichwa chake, awabariki, na Bikira Mtakatifu, katika wale ambao hawajapata mtu wa kuwakaribisha, daima awasindikize.