Katibu,UN:Kundi la nchi 77 ni Injini ya ushirikiano wa nchi zinazoendelea na maendeleo
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa III wa viongozi wa kundi la nchi 77 na China, uliofanyika tarehe 21 Januari 2024 mjini Kampala, Uganda alisema: “Msikubali kanuni mpya kwa ajili ya teknoloija mpya ziandikwe na matajiri kwa ajili ya matajiri. Bwana Guterres alisema ushiriki wa kundi hilo lenye wanachama 134 sasa kutokea nchi 77 waliokuwako miaka 60 kundi hilo lilipoundwa ni muhimu kwani hakuna sababu ya karne ya 21 kunakili ukosefu mkubwa wa usawa uliokuweko karne ya 20. Bwana Guterres alisisitiza kuwa teknolojia za kidijitali zina fursa kubwa ya kuleta mambo bora, lakini vile vile zinachochea ukosefu wa usawa. “Shirika la Fedha Duniani, linaonya kuwa Akili Mnemba (AI) inaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi.” Lakini “teknolojia mpya zinaweza kufanya kasi kubwa ufanikishaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs,” ambayo yanafikia ukomo wake 2030.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa adha alisema kuwa Mkataba pendekezwa kuhusu Matumizi ya Kidijitali Duniani, unalenga kuhakikisha katika zama mpya ya teknolojia ambayo hakuna mtu yeyote anayeachwa nyuma. Hivyo amesema ni matumaini yake kuwa mkataba huo uliopendekezwa utapitishwa wakati wa Mkutano wa Viongozi kuhusu Zama Zijazo, utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu 2024 jijini New York, Marekani. Aidha Katibu Mkuu wa UN amewajulisha kuwa Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu Akili Mnemba (AI) ambalo aliliunda mwaka 2023 likijumuisha wataalamu kutoka G77, ikiwa ni asilimia 50 ya nchi zinazoendelea na asilimia 50 ya nchi tajiri limewasilisha mapendekezo ya awali kuhusu usimamizi wa AI duniani na mchango wake katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs.) Bwana Guterres alipongeza nchini Cuba ikiwa ndiyo Rais wa G77 kwa kuweka sayansi na teknolojia kama jambo la kupatiwa kipaumbele na kundi hilo.
Katibu Mkuu wa UN hakuweza kuhitimisha hotuba yake bila kuzungumza mizozo inayoendelea duniani ikiwemo vita inayoendelea katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, (Hamas) kwa zaidi ya siku 100 sasa: “Mashariki ya Kati inawaka moto. Lazima tufanye kila tuwezalo kuzuia mzozo huo kusambaa ukanda mzima. Na hii ianze na sitisho la haraka la mapigano kwa sababu ya hadhi ya kiutu ili kupunguza machungu huko Gaza, na kuruhusu misaada ya kibinadamu kufikia kila mtu mwenye kuhitaji na kufanikisha kuachiliwa huru mateka wote haraka iwezekanavyo bila masharti yoyote.”
Katibu Mkuu vile vile alisema kuendelea kukataa hapo tarehe 20 Januari “kukubali suluhisho la mataifa mawili kwa Israel na wapalestina haikubaliki kabisa kama nilivyowaeleza viongozi wa Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote, NAM.” Kwa njia hiyo alirejea kauli yake kuwa kuendelea kuwanyima wapalestina haki ya kuwa na taifa lao kutaendeleza mzozo ambao tayari ni tishio la usalama na amani duniani; unaongeza mgawanyiko na kuibuka kwa misimamo mikali kila mahali. Katibu Mkuu alipongeza kundi hilo la nchi 77 na China akisema kuwa miongo kadha limekuwa Injini ya ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea na maendeleo, ikiinua mamilioni ya watu kutoka kwenye lindi la umaskini, na kuzipatia nchi zinazoendelea sauti kwenye jukwaa la kimataifa.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa UN alisema mamilioni ya wakazi walioko kwenye nchi hizo, bado wamekwama kwenye umaskini kutokana na madhara ya janga la Uviko-19, nchi zao zikiwa zinakwamishwa na madeni, gharama ya maisha ikiongezeka, sambamba na gharama za kukopa fedha. Kwa kuongeza Katibu wa UN alisema: “Madhara ya majanga ya tabianchi ambayo wengi wenu mmechangia kidogo sana kusababisha yamevuruga uchumi wenu na kuongeza machungu kwa watu.” Kwa kuongezea: “ ingawa ushirikiano wa nchi za kusini umekuwa thabiti na unaimarika ukitatua changamoto hizo, hii haichukui nafasi ya nchi tajiri kutekeleza ahadi zao za ushiriki endelevu wa kusaidia kutokomeza umaskini na kusaidia kujengea mnepo nchi zinazoendelea.”