Sherehe Ya Huruma Ya Mungu: Madonda Matakatifu Ya Kristo Yesu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sherehe ya Huruma ya Mungu. Mama Kanisa kwa hekima na busara yake, anataka watoto wake kuonesha moyo wa toba kwa kumwendea Padre anayemwakilisha Kristo Yesu katika kiti cha maungamo, Mahakama ya Huruma ya Mungu. Hii ndiyo njia sahihi ya kuweza kuonja na kupata: upendo, huruma na msamaha wa Mungu ambao kimsingi una mwelekeo pia wa kijamii, tayari kuponya madonda, mipasuko na kinzani za kijamii. Waamini wanakwenda kwenye kiti cha huruma ya Mungu si kwa kutaka kuhukumiwa, bali kukutana na hatimaye, kuambata upendo na huruma ya Mungu inayoendelea kuusimamisha ulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linalaani dhambi, lakini linamkumbatia mdhambi anayetambua dhambi zake na udhaifu wake tayari kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Kanisa halina budi kusamehe bila kuchoka kama anavyofundisha Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Mwenyezi Mungu yuko radhi kumpokea mwamini anayeonesha moyo wa toba na wongofu wa ndani, tayari kukumbatia na kuambata huruma ya Mungu. Kanisa lipo ili kuwawezesha waamini kukutana na huruma ya Mungu katika maisha yao.
Baba Mtakatifu anasema, ili Kanisa liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake, halina budi kutoka kwa kutambua kwamba, Kanisa ni kama hospitali kwenye uwanja wa vita, ambako linakutana na majeruhi wanaohitaji kusikilizwa, kueleweka, kusamahewa pamoja na kuonjeshwa upendo. Waamini wakaribishwe kwa heshima na taadhima wanapokimbilia huruma ya Mungu, bila kuwanyanyasa wala kuwakejeri. Upendo wa Mungu unaowakumbatia wadhambi wakati mwingine unaonekana kuwa ni kashfa mbele ya macho ya binadamu. Kristo Yesu anataka kuwaponya na kuwaokoa wale wanaoteseka kiroho na kimwili; tayari kuwaonjesha upendo na huruma ya Mungu. Waamini wanapaswa kushinda kishawishi cha kujiona kuwa ni watakatifu, wenye haki na wateule, bali watambue kwamba, ni wadhambi na wanahitaji kweli huruma na upendo wa Mungu.
Hapa Kanisa linapaswa kuwafungulia watu malango ya huruma ya Mungu katika ukweli na uwazi pasi na unafiki. Kanisa lisiwatwishwe watu mizigo mizito, bali liwaonjeshe waamini huruma ya Mungu pasi na kumezwa na malimwengu, uchu wa mali, fedha na pengine hata madaraka. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu inayotumika wakati huu wa Kipindi cha Pasaka, Kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 24 Aprili 2022, mwisho wa Oktava ya Pasaka, amejielekeza zaidi kwa Toma Mtume aliyekuwa “ametokomea kusikojulikana kwa muda wa siku nane pamoja na Kristo Yesu, ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu kwa binadamu. Toma Mtume, ni kielelezo cha waamini wote ambao hawakuwemo kwenye Chumba cha Juu, siku ile ya kwanza ya juma, Kristo Yesu alipowatokea wanafunzi wake milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi. Hata leo hii, kuna baadhi ya waamini wanayo mashaka makubwa kuhusu imani kwa Kristo Yesu Mfufuka anayeendelea kuwaambata katika maisha yao, hata kama bado hawajamwona wala kumgusa. Kuna waamini wanaotaka kuona ishara na miujiza kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na wafuasi wake, lakini mtindo huu wa maisha anasema, Baba Mtakatifu ni kielelezo cha uhaba wa imani “kama kiatu cha raba” kama ilivyokuwa kwa Toma, Mtume. Hakuna sababu ya kuona aibu kwani hakuna Mkristo ambaye ni mkamilifu katika imani yake.
Toma Mtume alikumbana na changamoto ya imani iliyomnyenyekesha, kiasi cha kukiri imani yake kwa Kristo Yesu, Ufunuo wa Uso wa Huruma ya Mungu. Changamoto ya imani inawawezesha waamini kutambua kwamba, wao daima ni wahitaji mbele ya Kristo Yesu, anayewaruhusu kuona na kugusa Madonda yake Matakatifu, ili kupyaisha uzoefu wa upendo wake wa daima, kama ilivyokuwa hapo awali. Ni heri kuwa na imani tenge inayosimikwa katika unyenyekevu, kwani inawawezesha kurejea tena kwa Kristo Yesu, anayewakirimia imani thabiti kuliko kuwa na imani inayomfanya mwamini kuwa na jeuri na kiburi, kaburi la utu na heshima yake. Kristo Yesu, kamwe hachoki kuwaendea waamini wake, kwani hakwaziki kwa udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu. Kristo Yesu anarejea tena na tena hata wakati ambapo milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; wakati wa hofu na mashaka, kwa sababu anatambua kwamba, waamini wanayo hamu ya kutaka kukutana naye katika hija ya maisha yao! Kristo Yesu anarejea ili kuwaonesha Madonda yake Matakatifu, alama ya upendo kwa udhaifu na mapungufu ya kibinadamu.
Kristo Yesu Mfufuka anapenda kurejea tena, ili aendelee kukaa pamoja na waja wake, lakini inategemea ikiwa kama wafuasi wake, wako tayari kumtafuta, ili kumwonesha udhaifu na mapungufu yao ya imani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Toma, Mtume. Kristo Yesu anarejea kwa sababu ni mvumilivu na mwingi wa huruma; yuko tayari kufungua malango ya woga, hofu na wasi wasi, kwa kuwapatia waja wake, fursa ya kuanza tena upya. Huu ni wakati kwa waamini kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia ni wepi katika safari ya maisha yao wamejitaabisha kumtafuta Kristo Yesu, au ni wakati gani walipothubutu kumfungia Kristo Yesu nje ya malango ya maisha yao. Changamoto hizi za kiimani, ziwawezeshe waamini kumwekea Kristo Yesu ahadi ya kumtafuta na hatimaye, kurejea kwake, ili kuambata: upendo, huruma na msamaha wake wa daima unaobubujika kutoka katika Madonda yake Matakatifu. Ni katika mwelekeo huu, waamini nao wanaweza kugeuka na kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu bila ya kuwa na shingo ngumu wala maamuzi mbele kwa madonda ya jirani zao.