Tafuta

Mwaka wa 728 Msamaha wa Papa Celestin: Huruma, Upendo Msamaha na Upatanisho wa Kweli

Ilikuwa ni tarehe 6 Aprili 2009 mji wa L’Aquila ulipokumbwa na tetemeko la ardhi, watu 309 wakapoteza maisha, wengine 1,600 kujeruhiwa na watu 80, 000 wakabaki bila makazi maalum baada ya nyumba zao kubomolewa. Baba Mtakatifu amewashukuru watu wote wa Mungu Jimbo kuu la L’Aquila kwa kuwezesha kufanikisha tukuo hili muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Agosti 2022 baada ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V, kwa kufungua lango la Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio” Jimbo kuu la Aquila, nchini Italia. Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ameonesha matumaini makubwa kwamba, mji wa L’Aquila utaweza kugeuka na kuwa ni mji mkuu wa: msamaha, amani na maridhiano. Baadaye, ameongoza Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio.” Amewashukuru watu wa Mungu waliohudhuria mubashara na wengine kushiriki tukio hili muhimu katika maisha ya kiroho kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, huku wakiwa wamelazwa hospitalini, wakiwa majumbani bila kuwasahau wafungwa wanaohitaji kwa namna ya pekee kuonja huruma, msamaha na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Papa Francisko amewapongeza watu wa Mungu kwa udugu na mshikamano
Papa Francisko amewapongeza watu wa Mungu kwa udugu na mshikamano

Ilikuwa ni tarehe 6 Aprili 2009 mji wa L’Aquila ulipokumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha watu 309 kupoteza maisha, watu wengine 1,600 kujeruhiwa vibaya na watu 80, 000 wakabaki bila makazi maalum baada ya nyumba zao kubomolewa na kutofaa tena kwa matumizi ya binadamu. Baba Mtakatifu amewashukuru watu wote wa Mungu Jimbo kuu la L’Aquila kwa kuwezesha kufanikisha tukuo hili muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.  Mchakato wa ukarabati wa mji wa L’Aquila umekwisha kuanza, lakini bado kuna kazi kubwa sana mbele ya wananchi wa L’Aquila; jambo la msingi ni kujenga ushirika na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili mji huu uweze kushuhudia tena tunu zake msingi yaani: Mahusiano na mafungamano ya kijamii bila kusahau shughuli zake za kiuchumi! Bado sehemu kubwa ya makazi ya wananchi yanapaswa kufanyiwa ukarabati mkubwa! Mjini kati, amana na utajiri wa mambokale umeharibiwa sana, lakini wafanyakazi wanaokarabati amana ya mambokale wameonesha matumaini makubwa ya kuweza kurejesha tena mji huu katika uzuri wake wa asili.

Ujenzi wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu ni muhimu.
Ujenzi wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu ni muhimu.

Kwa upande wake, Kardinali Giuseppe Petrocchi, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la L’Aquila, Italia, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuonesha na kushuhudia ukaribu wake kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la L’Aquila, Watatunza na kuhifadhi katika sakafu ya nyoyo zao, ujumbe makini aliowashikirisha katika maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V. Wataendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anapoongoza, fundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, huku akiendelea kuwasha moto wa furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Ni matumaini ya watu wa Mungu kwamba, kwa njia ya mwanga angavu wa Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium” yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko yatawasaidia walimwengu kupata neema, baraka na msamaha, chachu muhimu sana katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika ushirika na upatanisho wa kweli. Waamini wataendelea kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa kama alama ya ushirika, na jamii inayosimikwa katika tunu zinazoheshimu na kuthamini: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Tetemeko la ardhi
28 August 2022, 15:03

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >