Tafuta

Kristo Yesu ni Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu Kwa Waja Wake: Upendo Unaookoa

Ufunuo wa Mwenyezi Mungu unaokoa, unaganga na kumtibu mwanadamu kwa njia ya huruma na upendo wake usiokuwa na kikomo. Mwenyezi Mungu anatenda kwa njia ya upendo wake mkuuu. Huu ndio ushuhuda ambao wanafunzi wa Kristo Yesu wanatumwa kuutangaza na kuushuhudia kwa watu wa Mataifa kwamba, vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba Mwenyezi kwa binadamu wote ndiyo maana Kristo Yesu anamshukuru Baba yake wa mbinguni akisema: “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.” Mt 11:25. Ufunuo wa Mwenyezi Mungu unaokoa, unaganga na kumtibu mwanadamu kwa njia ya huruma na upendo wake usiokuwa na kikomo. Mwenyezi Mungu anatenda kwa njia ya upendo wake mkuuu. Huu ndio ushuhuda ambao wanafunzi wa Kristo Yesu wanatumwa kuutangaza na kuushuhudia kwa watu wa Mataifa kwamba, vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema ya Wokovu: Rej Mt 11:5. Huu ndio utukufu na ukuu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 9 Julai 2023, Dominika ya 14 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, ukuu wa Mungu hauwezi kufahamika wala kueleweka na watu wanaomuunda mungu wao wenyewe kwa sura na mfano wao; mungu mwenye nguvu, asiyebadilika na mwenye kulipiza kisasi. Kwa maneno mengine, hawa ni wale waliojawa na nafsi zao wenyewe, watu wenye kiburi, wanaojali masilahi yao tu, wanaojiaminisha kwamba hawahitaji mtu yeyote na wala hawawezi kumkaribisha Mungu kama Baba yao wa milele.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu

Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anasema: Ole wenu watu wa Korazini! Ole wenu watu wa Bethsaida! Ole wenu watu wa Kapernaumu. Kwa maana kama matendo makuu yaliyofanyika kwenye miji yenu yangelifanyika Tiro na Sidoni, watu wa huko wangelikuwa wametubu tangu zamani na kuvaa magunia na kujipaka majivu, kudhihirisha kujuta kwao. Rej Mt 11: 20-30. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kristo Yesu alijitaabisha kuwahubiria watu wa miji hii maarufu kwenye Agano Jipya, lakini wakazi wake, “wakapotezea mahubiri ya Kristo Yesu na ushuhuda wake.”  Kwa watu wale, miujiza ilikuwa ni matukio ya kuvutia yaliyotengeneza habari wakati huo na kuchochea “porojo na umbea”, mara tu masilahi yao ya mpito yalipotoweka, Habari Njema ya Wokovu ikihifadhiwa kwenye kumbukumbu na hivyo kushindwa kuyakaribisha mambo makuu ya Mungu katika maisha yao na hivyo kubaki wakavu kama “kigae.” Kristo Yesu anamshukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya aliwaficha wenye hekima na akili, akawafunulia watoto wachanga. Watu wadogo ni wale wanaojisikia kutoka katika undani wa maisha yao kuwa kama watoto wadogo, wasiokuwa na maamuzi mbele, watu wasiojitosheleza wenyewe, kumbe, wanahitaji uwepo na msaada wa Mungu, kiasi cha kushangazwa na matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Hawa ni watu wenye uwezo wa kusoma alama za nyakati na hivyo kushangazwa na miujiza ya upendo wake usiokuwa na kifani! Baba Mtakatifu anakaza kusema, maisha ya mwamini yamesheheni miujiza ya huruma, wema na upendo wa Mungu.

Maisha ya mwanadamu yamesheheni miujiza
Maisha ya mwanadamu yamesheheni miujiza

Lakini licha ya miujiza yote hii, nyoyo za waamini zinaweza kutoguswa hata kidogo, kiasi kwamba, miujiza yote hii inaonekana kuwa ni mambo ya kawaida na wala hakuna tena mshangao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mvuto ni kitenzi ambacho huleta akilini kuhusu filamu ya mpiga picha. Hapa kuna mtazamo sahihi mbele ya kazi za Mwenyezi Mungu: kupiga picha kazi zake katika akili, ili zichapishwe ndani ya moyo, na kisha kuziendeleza katika maisha, kwa njia ya ishara nyingi za wema, ili "picha" ya Mwenyezi Mungu inayofumbatwa katika upendo wake, uzidi kuangaza ndani ya waamini na kwa kupitia kwao. Mwishoni  mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawauliza waamini ikiwa kama katika “mafuriko” ya habari zinazowafikia, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa matendo makuu ya Mungu? Je, kama watoto wadogo katika hali ya ukimya wanaendelea kutenda mema ili kuleta mabadiliko katika sura ya nchi? Je, waamini wanao utamaduni wa kumshukuru Mungu kwa matendo yake makuu katika maisha yao? Bikira Maria aliyemtukuza Mwenyezi Mungu kwa ushuhuda wa maisha yake, awaombee waamini ili waweze kushangazwa na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani, ili hatimaye, waweze kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu katika hali ya kawaida.

Ufunuo wa upendo

 

09 July 2023, 15:29

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >