Tafuta

Papa Francisko Maadhimisho ya Siku ya Vijana 2027 Ni Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 yataadhimishwa Jimbo kuu la Seoul nchini Korea Kusini, kielelezo makini cha mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa na ndoto ya umoja na mshikamano wa watu wa Mungu, ndoto ambayo vijana wa kizazi kipya ni mashuhuda wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 Siku ya Vijana Ulimwenguni yatafanyika kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 3 Agosti 2025 Jimbo kuu la Roma: Mahujaji wa Matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 yataadhimishwa Jimbo kuu la Seoul nchini Korea Kusini, kielelezo makini cha mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa na ndoto ya umoja na mshikamano wa watu wa Mungu, ndoto ambayo vijana wa kizazi kipya ni mashuhuda wake.  Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na Siku ya 41 ya Vijana Ulimwenguni itaadhimishwa Jimbo kuu la Roma kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 3 Agosti 2025 kwa kunogeshwa na kauli mbiu Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kuhudhuria kwa wingi katika maadhimisho haya. Anasema, Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni 2027 ni Seoul Korea ya Kusini
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni 2027 ni Seoul Korea ya Kusini

Dominika tarehe 6 Agosti 2023 Sikukuu ya Kung’ara Bwana Yesu Kristo na ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno inayonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 6 Agosti, 2023 amekuwepo nchini Ureno. Itakumbukwa kwamba, hii imekuwa ni hija yake 42 ya Kimataifa na mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa “Parque Tejo”, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno, amewashukuru viongozi wa Kanisa, Serikali na Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni.

Vijana Mahujaji wa Matumaini 2027
Vijana Mahujaji wa Matumaini 2027

Baba Mtakatifu amewashukuru watu wakujitolea waliosadaka maisha yao kwa ajili ya huduma kwa vijana wa kizazi kipya, lakini shukrani za pekee zinamwendea Mtakatifu Yohane Paulo II Muasisi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni pamoja na watakatifu na wenyeheri wasimamizi na waombezi wa Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Amewashukuru na kuwapongeza vijana wa kizazi kipya jinsi wanavyopendeza na kwamba, ni Mwenyezi Mungu peke yake anayefahamu kile ambacho amepandikiza nyoyoni mwao. Jambo la msingi ni vijana kuendelea kukumbuka Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Watunze ndani mwao, matukio makuu yaliyoacha chapa ya kudumu katika sakafu ya nyoyo zao, kamwe wasikatishwe tamaa na uchovu, bali waendeleee kutunza ndani mwao baraka na neema ya Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, tayari kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika wao ni watu wa Mungu wanatumwa kutangaza furaha ya Injili. Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee vijana wote ambao hawakuweza kuhudhuria katika maadhimisho haya kutokana na sababu mbalimbali, vijana wote walioshiriki maadhimisho haya kwa ngazi ya kijimbo na kwenye Makanisa mahalia, kwa mfano vijana walioshiriki maadhimisho haya huko Tangier. Baba Mtakatifu amewakumbuka vijana ambao hawakuhudhuria kutoka na vita na kwamba, ndani mwake anayo ndoto ya amani, vijana wakisali kwa ajili ya kuombea amani, wakiishi katika amani pamoja na kujenga kesho yao kwa njia ya amani. Bikira Maria, Malkia wa Amani aendelee kuwaombea walimwengu amani, ili watu waweze kuthamini tofauti zao msingi za utaifa, lugha na historia mambo yanayopaswa kuwaunganisha kuliko kuwagawa! Baba Mtakatifu amemshukuru Kristo Yesu na Bikira Maria ambao wamekuwepo daima katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni.

Seoul Korea ya Kusini
06 August 2023, 14:44

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >