Kupashwa Habari Bikira Maria Kuwa Atakuwa Ni Mama wa Mungu! UVULI!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, Kristo Yesu alitungwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu akazaliwa na Bikira Maria na huo ndio utimilifu wa nyakati. Bikira Maria ameitwa kumchukua mimba yule ambaye ndani yake “utimilifu wote wa Kimungu utakaa kwa jinsi ya kimwili.” Jibu la Mungu kwa swali lake “litakuwaje neno hili, maana simjui mume?” Limetolewa kwa uweza wa Roho Mtakatifu: “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako. Roho Mtakatifu ambaye ni Bwana na mleta uzima anatumwa kutakatifuza tumbo la uzazi la Bikira Maria na kulirutubisha Kimungu, na hivi kumfanya achukue mimba ya Mwana wa milele wa Baba katika ubinadamu uliochukuliwa kutoka kwake. Mwana wa pekee wa Baba, akiwa amechukuliwa mimba kama mtu, katika tumbo la Bikira Maria, ndiye “Kristo”, yaani aliyepakwa na Roho Mtakatifu tangu mwanzo wa uwepo wake wa kibinadamu, hata kama kuoneshwa kwake kumetokea hatua kwa hatua: kwa wachungaji, kwa Mamajusi, kwa Yohane Mbatizaji na kwa wafuasi wake. Maisha yote ya Kristo Yesu yatamwonesha jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu. Imani juu ya Bikira Maria ina msingi wake juu ya Kristo Yesu na kuangazia imani yake katika Kristo Yesu. Bikira Maria alichaguliwa tangu milele yote kuwa ni Mama wa Kristo Yesu kwa kumkingia dhambi ya asili. Rej. KKK 484-507.
Kanisa katika Dominika ya IV ya Kipindi cha Majilio linaweka mbele ya macho ya waamini utabiri wa kuzaliwa kwake Kristo Yesu: “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.” Lk 1:26-38.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 24 Desemba 2023 amejikita zaidi katika kipengele kinachozungumzia kuhusu: “nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli.” Katika nchi kama ile ya Bikira Maria yenye jua kali daima, mti unaostahimili ukame na kutoa kivuli ni kielelezo cha ukarimu, kitulizo na ulinzi. Kivuli ni zawadi ambayo huburudisha na Malaika anabainisha kwa usahihi njia ambayo Roho Mtakatifu atashuka na kukaa juu ya Bikira Maria; njia ya Mwenyezi Mungu yakutenda mambo husimikwa katika upendo, upole unaokumbatia na kuambata; kurutubisha na kulinda bila ya kufanya vurugu wala kuumiza uhuru wa mtu. Kivuli ni wazo linalotawala katika Maandiko Matakatifu, Waisraeli walipokuwa Jangwani, Mwenyezi Mungu aliwaongoza ndani ya wingu mfano wa nguzo; Jibu la Mwenyezi Mungu kutokana na manung’uniko ya Nabii Yona: “Na BWANA Mungu aliweka tayari mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango. Lakini siku ya pili kulipopambazuka, Mungu akaweka tayari buu, nalo likautafuna ule mtango, ukakatika. Basi ikawa, jua lilipopanda juu, Mungu akaweka tayari upepo wa mashariki, wenye hari nyingi; jua likampiga Yona kichwani, hata akazimia, naye akajitakia kufa, akasema, Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi. Mungu akamwambia Yona, Je! Unatenda vema kukasirika kwa ajili ya mtango? Naye akasema, Ndiyo, natenda vema kukasirika hata kufa. Bwana akamwambia, Wewe umeuhurumia mtango, ambao hukuufanyia kazi, wala kuuotesha; uliomea katika usiku mmoja, na kuangamia katika usiku mmoja; na mimi, je! Haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi ya mia na ishirini elfu, wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto; tena wamo wanyama wa kufugwa wengi sana? Yon 4:6-11. Mwenyezi Mungu ni kinga kuu ya waadilifu: “Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.” Zab 91:1. Kimsingi kivuli kinazungumzia wema na ukarimu wa Mungu.
Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu alivyomtendea Bikira Maria, na anavyoendelea kutenda kwa kutoa kimbilio na kitulizo, mwaliko wa kumwendea na kukaa na Mwenyezi Mungu. Hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu wenye kuzaa matunda mema na kwamba, waamini wanaweza kupata mang’amuzi yake, yaani kati ya; marafiki, wachumba, wanandoa, wazazi na watoto wanapojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na heshima ya wahusika; na kwa ajili ya tunza ya wengine kwa wema. Hivi ndivyo anavyopenda Mwenyezi Mungu na anatoa mwaliko kwa waja wake kutenda kama anavyotenda, kwa kuwakarimu, kuwalinda na kuwaheshimu wengine. Katika kipindi hiki cha Noeli, watu watakusanyika: Makanisani, barabarani, watakutana na jirani pamoja na marafiki waliopoteana kwa muda mrefu, lakini hata katika hali na mazingira kama haya, bado kutakuwepo na wale watakaoadhimisha Noeli ya Bwana katika hali ya upweke. Hizi ni fursa wa kutenda wema kwa: kusikiliza, kusindikiza na kutembelea ili kuwatengenezea wengine “kivuli cha Aliye juu” ili kiwafunike. Katika maadhimisho haya ya Noeli ya Bwana, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kutoa nafasi kwa uvuli wa Roho Mtakatifu, kwa upole wa Mwenyezi Mungu, kwa kumtengenezea nafasi rohoni mwao, kwa kukaribia katika Sakramenti ya Upatanisho ili kuonja msamaha wake pamoja na Ekaristi Takatifu. Waamini wawe ni kivuli kinachorejesha urafiki unaofariji. Wamwombe Bikira Maria ili awasaidie kuwa wazi na hivyo kukaribisha uwepo wa Mungu anayekuja kuwaokoa kwa upole na unyenyekevu.