Papa Francisko:Kazi ya dini ni kuwa mfano mzuri kwa ajili amani na tabianchi
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Kuunda miunganisho kwa ajili ya manufaa ya wote. Ni moyo wa ujumbe kwa njia ya video ambao Baba Mtakatifu Francisko ameutuma huko Dubai akielezea juu ya masikitiko yake ya kutokuwepo kwenye hiyo COP28 na kumkabidhi tena Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, kile alichokiandaa kwa ajili ya uzinduzi wa "Faith Pavillon" yaani “Banda la Imani.” Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza umuhimu wake kwani hiyo ni kwa mara ya kwanza kwa banda la kidini kuundwa ndani ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Ulimwengu unahitaji miunganisho kwa ajili ya maslahi ya kila mtu. Katika ukweli ambao COP28 inayoendelea katika Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu inakaribisha Banda la Imani ambapo ni ishara ya kutaka kuonesha kwamba inawezekana kuunda miungano yenye faida kwa ajili ya maslahi ya pamoja. Miongoni mwa haya Papa anasema “ya muhimu zaidi leo ni amani na hali ya tabianchi." “Leo dunia inahitaji miungano ambayo si dhidi ya mtu yeyote, bali kwa kila mtu. Ni jambo la dharura kwamba dini, bila kutumbukia katika mtego wa ulinganifu, ziweke mfano mzuri kwa kufanya kazi pamoja: si kwa maslahi yao wenyewe au ya chama kimoja, bali kwa ajili ya maslahi ya ulimwengu wetu.
Kwa siku zijazo hasa za watu walio hatarini zaidi na mustakabali wa wote, himizo la Papa Francisko ni kulinda kazi ya uumbaji na kulinda nyumba yetu ya pamoja. Kwa hiyo Papa ametoa mwaliko kuwa, “Tuishi kwa amani na kuendeleza amani!" Aidha Papa amesema kuwa "Tunaongoza kwa mfano, kama wawakilishi wa kidini, kuonesha kwamba mabadiliko yanawezekana, kutoa ushuhuda wa maisha ya heshima na endelevu, na tunaomba kwa sauti kubwa viongozi wa mataifa kwamba nyumba ya pamoja ihifadhiwe. Hili linaombwa kwetu, hasa, na watoto na maskini, ambao maombi yao yanafikia kiti cha enzi cha Aliye Juu."
Banda la kwanza la Imani litakuwa kipaumbele ili kuwa kitovu cha kukuza ushirikiano na umoja wa imani kati ya dini mbalimbali, kwa lengo la kuchochea hatua madhubuti na kabambe ya hali yatabianchi. Litaunda fursa ya mazungumzo na wawakilishi wa kidini na wazalendo, wanasayansi, vijana na viongozi wa kisiasa ili kuharakisha hatua za hali ya tabianchi. litakuwa mwenyeji zaidi ya vikao 60, vinavyowakilisha zaidi ya mashirika 100.