Nyumba ya Sala Ni Kielelezo Cha: Uwepo, Ukaribu Ili Kujenga Umoja na Udugu wa Kibinadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Ni katika muktadha wa utakaso wa Hekalu. Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa ni nyumba ya biashara. Rej. Yn 2: 13-25. Kwa hakika nyumba ya Mungu ilikuwa imegeuzwa kuwa ni soko. Soko na nyumba ya sala ni mambo mawili yanayokinzana, ili kukutana na Mwenyezi Mungu. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 3 Machi 2024, Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Kwaresima, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana iliyotolewa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, hapa hekalu likimaanisha soko, ilikuwa ni sehemu ya kununua kondoo, ukalipa na kuanza kula pembeni mwa altare: Kumbe, maneno makuu yanayochukua uzito wa pekee hapa ni: kununua, kulipia na hatimaye, kula, na baada ya hapo, kila mtu alirejea nyumbani mwake, ili kuendelea na shughuli za kawaida. Lakini hekalu likiwa na maana ya “Nyumba ya Sala” linachukua maana tofauti kabisa, kwani hapa ni mahali ambapo mwamini anakwenda ili kukutana na kuongea na Mwenyezi Mungu; ili kukaa na waamini wengine, ili kushirikishana furaha na majonzi katika maisha.
Sokoni ni mahali ambapo kinachoangaliwa zaidi ni bei, lakini nyumbani, hakuna malipo; sokoni mtu anatafuta mafao yake binafsi, lakini nyumbani hii ni sadaka na majitoleo kamili. Kristo Yesu katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu anaonekana kuwa mkali kabisa kiasi kwamba, hakubaliani hata kidogo watu kugeuza nyumba ya Baba yake kuwa kama soko, kwani kama soko, linaonesha mahusiano na mafungamano ya mbali kabisa na Mwenyezi Mungu. Nyumba ya sala, ni kielelezo cha uwepo wa karibu wa Mungu kwa waja wake, mahali wanafamilia wanapokusanyika kwa ajili ya mlo wa pamoja ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu. Lakini dhana ya soko inakinzana na tunu msingi za maisha ya kiroho kiasi cha kujenga ukuta kati ya Mungu na binadamu na kati ya mtu na jirani yake, wakati ambapo Kristo Yesu amekuja ulimwenguni ili kujenga na kudumisha ushirika, huruma na ukaribu. Wito mahususi kwa waamini katika kipindi hiki cha Kwaresima ni kujibidiisha kujenga Hekalu kuwa ni nyumba ya sala, kwa kusali bila kuchoka, kwa kuwa na imani na Mwenyezi Mungu pamoja na kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Ni wakati wa kukuza na kudumisha ukimya mtakatifu, lakini huu si ule ukimya wa kutisha ambao watu wanautengeneza wakiwa kwenye usafiri wa umma, humo kila mtu anajikuta akiwa amezama katika mawazo yake, machungu na magumu yanayomkabilia kama mtu binafsi. Ni watu wanaozama kwenye simu za kiganjani.
Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, watu wamefikia mahali ambapo hawawezi kutoa tabasamu au kuchangia mawazo kwa jirani zako! Lakini kwanini binadamu atumbukie katika mwelekeo kama huo? Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kupiga hatua ya kwanza kwa kuwsalimia jirani zao, wajenge ujasiri wa kuzungumza na yule ambaye yuko karibu nao, ingawa hata wakati mwingine, hawataweza kupata jibu makini na watu hawa wanaweza kuwaangalia kwa jicho baya zaidi, walau lakini watakuwa wamejitahidi kujenga nyumba! Uelewa huu unaweza kutumika hata katika mazingira mbalimbali ya maisha ya kila siku. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiuliza maisha yao ya sala yako namna gani? Je, ni gharama ya kulipia au ni tabia ya mwamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu? Je, wamekuwa ni watumwa wa muda katika kusali? Je, mahusiano na mafungamano yao na jirani zao yako namna gani? Je, wanaweza kujisadaka bila ya kujibakiza bila kutegemea kurudishiwa fadhila? Je, wamekuwa ni watu wa kwanza kuvunjilia mbali kuta za ukimya sanjari na kujenga madaraja ya kuwakutanisha na wengine?