Tafuta

Saa ya Yesu: Utukufu wa Kristo Yesu Umetundikwa Juu ya Msalaba

Papa Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 17 Machi 2024 amekazia kuhusu: Utukufu wa Kristo Yesu ulivyotundikwa Msalabani unafumbata sadaka na msamaha wa dhambi; sadaka inayotolewa kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Utukufu wa Msalaba ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu kwa njia ya matedo, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Tano ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka B wa Kanisa ni mwaliko wa kujiandaa kushiriki katika ile Saa ya Kristo Yesu, yaani ile Saa ya Msalaba na mateso, ambayo kwa hiyari yake mwenyewe, anaamua kujitosa kimasomaso kuteswa na kufa Msalabani na hatimaye, kufufuka siku ya tatu kama ilivyoandikwa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ndio mwanzo wa Injili unaojikita katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Wasifu wa watu maarufu katika ulimwengu huu unaanza kwa siku yake ya kuzaliwa hadi pale anapoitupa mkono dunia! Lakini, kwa Yesu, wasifu wake unaanza katika mateso, kifo na ufufuko wake. Hii ndiyo amana na hazina ya imani ambayo vijana wa kizazi kipya wanapaswa kurithishwa, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa. Kifo cha Kristo Yesu kimetokana na dhambi za binadamu, na Saa yake ni wakati wa kukinywea kile Kikombe cha mateso. Mateso ya Kristo Yesu yanawahusisha watu wengi: Yuda Iskarioti aliyemsaliti kwa busu! Mtakatifu Petro aliyemkana mara tatu, Mitume waliotimua mbio walipoona amekamatwa na kukokotwa kuelekea hukumuni, Pilato aliyenawa mikono akisema hausiki kabisaaa na kifo cha Yesu, hata kama hakumkuta na hatia, lakini amestahili kufa! Huu ndio mwelekeo wa wale wanaopindisha sheria kwa ajili ya mafao yao binafsi! Baraba anayeponea chupu chupu kutoka katika tundu la sindano! Wevi wawili waliokuwa wametundikwa Msalabani. Yote haya ni maandalizi ya kuingia Juma kuu, fursa ya kutafakari juu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Huu ni muda wa kufunika Misalaba na Sanamu Makanisani hadi Ijumaa kuu na Sanamu katika mkesha wa Pasaka.

Utukufu wa kristo Yesu Umetundikwa Msalabani
Utukufu wa kristo Yesu Umetundikwa Msalabani

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 17 Machi 2024 amekazia kuhusu: Utukufu wa Kristo Yesu ulivyotundikwa Msalabani unafumbata sadaka na msamaha wa dhambi; sadaka inayotolewa kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Baba Mtakatifu anasema: Utukufu wa Msalaba ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba kwa binadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. “Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.” Yn 12: 23-24.

Maandalizi ya Juma Kuu: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu
Maandalizi ya Juma Kuu: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu

Utukufu wa Mungu ni tofauti kabisa na utukufu pamoja na umaarufu wa kibinadamu. Utukufu wa Mungu ni kupenda na kujisadaka kiasi hata cha kuyamimina maisha kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo; ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu, kwa kusadaka maisha pamoja na kuwasamehe watesi wake. Msalaba ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anafundisha utukufu wa kweli usiofifia, chemchemi ya furaha inayofumbatwa katika sadaka na msamaha, kiini cha utukufu wa Mungu. Sadaka na msamaha ni mambo yanayosimikwa katika kutoa kuliko kupokea. Utukufu wa kibinadamu ni jambo linalopita bila kuacha furaha ya kweli, ustawi na mafao ya wengi na matokeo yake na mipasuko, kinzani, chuki na uhasama. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kuwaulizia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, Je, ni utukufu upi wanaofikiria kwa ajili ya maisha yao ya sasa na yale ya mbeleni; Je, watu wengine wanayaonaje mafanikio au mambo wanayomiliki kwa sasa? Je, njia ya sadaka na msamaha, iliyooneshwa na Kristo Yesu; Njia ambao kamwe haichoki kupenda ni amini na kwamba, hii ndiyo njia ambayo imeshuhudiwa na Mungu, Je, inaoonesha na kushuhudia uzuri wa maisha. Waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, pale wanapojitahidi kujisadaka na kusamehe, utukufu wa Mungu unachanua na kung’ara. Bikira Maria aliyemfuata Kristo Yesu kwa imani katika ile Saa yake ya mateso, kifo na ufufuko, awasaidie waamini kuwa kweli ni mng’ao wa upendo hai wa Kristo Yesu.

Papa Saa ya Yesu
17 March 2024, 14:19

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >