Tafuta

Dominika ya Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa

“Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara... Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; ... Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo wangu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa. Huu ni mwaliko wa kutafakari juu ya zawadi ya thamani kubwa ambayo Kristo Yesu anamkirimia kila mwamini, tayari kushiriki katika mpango wake wa upendo, unaomwalika kila mwamini kuhakikisha kwamba, anamwilisha ndani mwake uzuri na tunu msingi za Injili katika hali zote za maisha. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa unanogeshwa na kauli mbiu: “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani.” Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu watu walioko safarini mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana na kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Sala kwa ajili ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 anasema, sala ndiyo nguvu na ufunguo wa malango ya matumaini. Waamini ni mahujaji wa matumaini na wajenzi wa amani na kwamba, lengo kuu la safari ya maisha ni kuishi kwa haki, amani na upendo na kwamba, lengo na wito ni kwa waamini kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; umoja, amani na udugu. Kila mwamini ajitahidi kugundua wito wake sahihi katika Kanisa na Ulimwengu, kwa kuwa hujaji wa matumaini na wajenzi wa amani.

Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa
Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, 21 Aprili 2024 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema kwamba Kristo Yesu anasema: “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si mali kitu kwake. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.” Yn 10: 11-15. Kristo Yesu anakazia kuhusu kuutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, nyakati za Kristo Yesu uchungaji haukuwa ni kazi peke yake, bali ni maisha yaliyowalazimu wachungaji kuambatana na mifugo yao siku nzima: mchana na usiku. Yesu anasema Yeye si mtu wa mshahara ambaye mambo ya kondoo si mali kitu kwake. Kristo Yesu anajitambulisha kuwa ni mchungaji mwema anayewajua kondoo wake nao wanamjua; anawaita kwa majina, anajitaabisha kuwatafuta pale wanapopotea. Kristo Yesu ni mchungaji mwema aliyeyamimina maisha yake, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu na hatimaye, akawakirimia waja wake Roho Mtakatifu.

Dominika ya Mchungaji mwema, Siku ya 61 ya Kuombea Miito 2024
Dominika ya Mchungaji mwema, Siku ya 61 ya Kuombea Miito 2024

Kristo Yesu ni kiongozi mkuu wa kondoo wake anayewajali kondoo wake kama kielelezo cha upendo katika maisha yake, changamoto na mwaliko kwa waamini kutambua thamani kubwa ya maisha yao mbele ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Je, waamini ndani mwao, wanatambua uzuri huu au wakati mwingine wanashindwa kuutambua uzuri huu. Hata leo hii kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, hawafai “hata kufua dafu” au pengine wanadhani kwamba, “wamekosea njia” kwa kuangalia ufanisi wa malengo yao katika maisha au maamuzi kutoka kwa watu wengine, kiasi cha kujikatia tamaa ya maisha, lakini, leo Kristo Yesu anapenda kuwakumbusha wafuasi wake kwamba, wanayo thamani kubwa sana mbele yake, jambo la msingi ni wao kujiweka chini ya mikono yake, Yeye ambaye ni Mchungaji mwema. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujitengea muda wa kuweza kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu Mchungaji mwema katika: Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu; kwa kumsifu na kumtukuza, ili hatimaye, mwamini aweze kumwachia nafasi Kristo Yesu Mchungaji mwema, aweze kumbembeleza na kwa njia hii, mwamini ataweza kugundua siri ya maisha. Jambo la msingi kwa waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, Kristo Yesu amateswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili yao na kwamba, kila mwamini ni mtu muhimu sana mbele ya Yesu Mchungaji mwema. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie waamini kumtambua Kristo Yesu kuwa ni muhimu sana katika maisha yao.

Siku ya 61 ya Kuombea Miito
21 April 2024, 14:49

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >