Jumatatu Oktava ya Pasaka: Furaha Shirikishi ya Ufufuko wa Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, inayotumika katika kipindi hiki cha Pasaka amegusia kwa namna ya pekee kabisa ile furaha ya kuwashirikisha wengine Habari Njema ya Wokovu, Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ni tukio lililoleta mabadiliko makubwa katika historia na maisha ya watu na kwamba, wakristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashirikishwa pia ile furaha ya Kristo Mfufuka kwa kuifia dhambi

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Tarehe Mosi Aprili 2024 Mama Kanisa anaadhimisha Jumatatu ya Oktava ya Pasaka. Hii pia ni Siku ya Malaika, kwani ni ile siku ambayo Malaika alikutana na wale wanawake waliokwenda kaburini alfajiri na mapema, siku ya kwanza ya juma. Walipotaza waliona kuwa lile jiwe limekwisha kuviringishwa, wakaingia, wakamwona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe. “Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.” Mk 16:6-7. Kwa hakika wanawake hawa walikuwa na furaha kubwa isiyokuwa na kifani kuhusu Habari Njema ya Ufufuko wa Kristo kwa wafu, kiasi cha kuondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Hii ni furaha inayobubujika moyoni mwa mwamini baada ya kukutana na Kristo Yesu Mfufuka na hiyo inakuwa ni changamoto ya kutoka mbio kwenda kutangaza na kushuhudia kile walichoona kwa macho yao. Ni katika muktadha wa furaha ya wanawake waliokutana na Kristo Mfufuka, Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, inayotumika katika kipindi hiki cha Pasaka amegusia kwa namna ya pekee kabisa ile furaha ya kuwashirikisha wengine Habari Njema ya Wokovu, Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ni tukio lililoleta mabadiliko makubwa katika historia na maisha ya watu na kwamba, wakristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashirikishwa pia ile furaha ya Kristo Mfufuka.

Kwa Ubatizo waamini wanashirikishwa furaha ya Kristo Mfufuka
Kwa Ubatizo waamini wanashirikishwa furaha ya Kristo Mfufuka

Baba Mtakatifu anasema, furaha ya ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ni mang’amuzi na uzoefu mzito katika maisha. Hali hii inaweza kujionesha kwa mwanafunzi aliyefaulu vyema masomo yake, mwanamichezo aliyefanikiwa kupata tuzo katika maisha, au familia iliyopata zawadi ya mtoto mchanga. Hizi ni nyakati ambazo wakati mwingine, inakuwa ni vigumu kuweza kuzisimlia kwa maneno, inagawa mara nyingi zina hamasisha watu kuzishirikisha haraka iwezekanavyo. Wanawake waliokutana na Kristo Mfufuka walikuwa na furaha kubwa kupita kiasi kwa sababu ya kukutana na Kristo Mfufuka, Habari Njema ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika historia ya maisha ya mwanadamu. Ufufuko kwa wafu ni ushindi wa Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo; Ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya matumaini na faraja. Kwa njia ya ufufuko wake, Kristo Yesu amevunjilia mbali nguvu za giza, dhambi na mauti na sasa anaishi milele yote.

Ufufuko wa Kristo Yesu ni kiini cha imani ya Kanisa
Ufufuko wa Kristo Yesu ni kiini cha imani ya Kanisa

Kumbe, kwa kuungana na Kristo Yesu, kila siku inakuwa ni hatua ya kuelekea maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Wakristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki ile furaha ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kwa waamini kama ilivyokuwa kwa wale wanawake, wana uwezo wa kukutana naye mubashara na kuwaambia “msiogope.” Kristo Yesu ameshinda dhambi na woga. Huu ni mwaliko kwa waamini kukita maisha yao katika matumaini, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Kristo Mfufuka na kwamba, furaha ya Kristo Mfufuka ndiyo injini ya maisha. Kristo Mfufuka ni chemchemi ya furaha isiyoweza kukauka hata kidogo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujibidiisha kumtafuta Kristo Mfufuka katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Upatanisho ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na kifani; katika Sala na upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Furaha ya Kristo Mfufuka inatangazwa, inashuhudiwa na kuwashirikisha wengine na kwa jinsi hii, furaha hii inaongezeka. Bikira Maria anayefurahi katika kipindi hiki cha Pasaka kwa sababu Mwanye mpendwa amefufuka kwa wafu, awasaidie waamini kuwa ni mashuhuda wenye furaha kwa Kristo Mfufuka.

Oktava ya Pasaka

 

01 April 2024, 14:47

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >