Maadhimisho ya Dominika ya Huruma ya Mungu: Imani, Upendo na Matumaini

Maadhimisho ya Dominika ya Huruma ya Mungu, tarehe 7 Aprili 2024, Papa Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amekazia kuhusu ushuhuda wa wanafunzi wa Yesu na imani ya kwamba, “Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.” Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu ni chemchemi ya : furaha, upendo na matumaini na wajibu wa kukutana na Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Huruma ya Mungu daima ni aminifu na inasimikwa katika uvumilivu, chemchemi ya ufufuko wa Mitume wa Yesu, waliomkana na kumkimbia wakati wa mateso na kifo chake Msalabani. Huruma na msamaha ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu na maisha ya Mwenyezi Mungu. Katika Injili ya Luka, 6:37, Yesu anasema “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Naye Mtakatifu Yakobo, Mtume katika Waraka wake anasema, “Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu. Waamini wanaalikwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Madonda yake Matakatifu, ili Kristo Mfufuka aweze kuwaimarisha katika imani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Tomaso, Mtume, kielelezo cha wakristo wanaohangaika na kutanga tanga katika imani yao! Dominika ya Pasaka, Kanisa limeadhimisha Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Dominika ya Huruma ya Mungu ni ufufuko wa Mitume wa Yesu kutoka katika hofu, woga na mashaka yaliyowafanya kujifungia ndani kwa kuogopa “kipigo cha Wayahudi.” Mitume bado walikuwa na mashaka kuhusu Ufufuko wa Kristo kwa wafu. Katika kipindi hiki cha patashika nguo kuchanika, Mtakatifu Tomaso, Mtume, hakuwepo, kwani waswahili wanasema “eti alikua ametokomea mahali pasipojulikana.” Katika muktadha huu, Kristo Mfufuka anawatokea wanafunzi wake, milango ikiwa imefungwa kwa hofu ya Wayahudi na kusimama kati kati yao na kuwaambia “Amani iwe kwenu.” Huu ni mwanzo wa huruma ya Mungu ambayo daima ni aminifu na inasimikwa katika uvumilivu. Mwenyezi Mungu kamwe hachoki kuwanyooshea mikono yake, ili kuwasimamisha tena wale walioteleza na kuanguka. Waamini wanapaswa kumwangalia Mwenyezi Mungu kama Baba mwenye huruma. Anatambua fika uwepo wa dhambi na udhaifu wa moyo unaomwangusha mara kwa mara mwanadamu. Mwenyezi Mungu anaweza kuwainua tena waja wake kwa mkono wa huruma, kwani bila huruma yake, mwanadamu hawezi kufua dafu wala kusimama kwa miguu yake mwenyewe!

Dominika ya Huruma ya Mungu
Dominika ya Huruma ya Mungu

Mwanadamu katika hija yake ya maisha, daima ataendelea kuteleza na kuanguka, lakini, huruma ya Mungu itamshika mkono na kumwinua tena. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anawaangalia watoto wake walioanguka na kumezwa na malimwengu, lakini anawaangalia kwa jicho la huruma, ili waweze kusimama tena na kusonga mbele! Mwenyezi Mungu anawapenda watoto wake kwa upendo wenye huruma. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa la “Santo Spirito in Sassia” kwa sasa limegeuka kuwa ni Madhabahu ya Huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Roma. Hii ni kumbukumbu endelevu katika historia na maisha ya Kanisa, kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kuanzisha Dominika ya Huruma ya Mungu katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo. Huu ni mwaliko kwa waamini kuupokea ujumbe wa huruma ya Mungu kwa imani na matumaini makubwa kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska alipoambiwa kwamba, Kristo Yesu ni upendo na huruma; na wala hakuna dhambi kubwa kiasi gani inayoweza kushinda huruma ya Mungu. Hii ni huruma inayonafsishwa katika sadaka na majitoleo bila ya kujibakiza hata kidogo. Kristo Yesu anawataka waamini kusadaka dhambi na udhaifu wao wa moyo; kwa kumwonesha jinsi ambavyo wameteleza na kuanguka dhambini. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Dominika ya Huruma ya Mungu, tarehe 7 Aprili 2024, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amekazia kuhusu ushuhuda wa wanafunzi wa Yesu na imani ya kwamba, “Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.” Yn 20:31; Kristo Yesu akawaonesha Madonda yake Matakatifu na kuwakirimia furaha, upendo na matumaini, mwaliko kwa waamini kujibidiisha kukutana na Kristo Yesu pamoja na kuamini nguvu ya Ufufuko wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anasema, kuna namna nyingi ya kuwa na uzima: kwa kumiliki mambo mengi, kwa kunywa na kula, kwa kuwa na fedha nyingi, lakini yote haya hayawezi kuuridhisha moyo, kwani uchu wa mali, madaraka na anasa ni mambo ambayo kamwe hayawezi kumpatia mwamini furaha ya kweli.

Huruma ya Mungu ni chemchei ya furaha, imani, matumaini na mapendo
Huruma ya Mungu ni chemchei ya furaha, imani, matumaini na mapendo

Kuna mambo mengine yanayogusa na kutikisa maisha ya watu, kwa mfano upendo, udhaifu wa mtu na hatimaye, kifo; matumaini ya kuishi milele na kupendwa pasi na ukomo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini ili kuwa na maisha mapya lazima wamwangalie Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka; washiriki kikamilifu katika maisha ya Kisakramenti; kwa kukuza na kudumisha maisha ya sala, kwa kutambua uwepo wake na hivyo kutoa neema na baraka zake ziweze kuwaongoza katika hija ya maisha yao hapa duniani; kwa kupenda kama Kristo Yesu anavyopenda. Mkutano wowote na Kristo Yesu unasaidia kuwa na utimilifu wa naisha. Baba Mtakatifu anatumia fursa hii kuwauliza waamini Je, wana amini juu ya nguvu ya Ufufuko kwa wafu, ushindi wa Yesu dhidi ya dhambi, hofu na katika kifo. Je, mwamini anajibidiisha kutafuta mafungamano na mahusiano ya dhati kabisa na Kristo Yesu katika maisha yake. Je, Kristo Yesu anampigania ili aweze kupenda kama Kristo Yesu alivyowapenda wao. Mwishoni Baba Mtakatifu amewaalika waamini kumwomba, Bikira Maria aweze kuwaombea imani thabiti ya ufufuko wa wafu kwa ajili ya maisha, tayari kutangaza na kueneza furaha ya Pasaka. Kristo Yesu anawataka watubu na kumwongokea kwa kuacha dhambi; kwa kuondokana na makovu ya majeraha yaliyopita; kwa kuondoa chuki na hasira dhidi ya jirani zao pamoja na hali ya kuwadhania wengine vibaya! Kristo Yesu anaendelea kuwasubiri waja wake, ili wamwendee na kumpelekea dhambi na udhaifu wa moyo, tayari kugundua chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani!  Mtume Tomaso aliyekuwa amechelewa, lakini anapokumbatia huruma ya Mungu, anakuwa wa kwanza na hivyo kuwapita Mitume wengine wote. Anakiri na kuungamana imani katika Fumbo la Ufufuko na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa kusema “Bwana wangu na Mungu wangu.” Huu ndio ufufuo wa Mtume anayetambua dhambi na udhaifu wake wa moyo unaopenya na kuingia ndani ya Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Hofu na mashaka yakatoweka na Mwenyezi Mungu akawa ni “Mungu wangu.” Huu ni mwanzo wa Mtume kujikubali jinsi alivyo na kuanza kujipokea, kiasi hata cha kuyapenda maisha yake!

Dominika ya Huruma ya Mungu chemchemi ya imani na matumaini
Dominika ya Huruma ya Mungu chemchemi ya imani na matumaini

Binadamu wote ni sawa na ni dhaifu lakini wote wana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Huu ni wakati wa kung’oa vitendo vyote vinavyosababisha mifumo mbali mbali ya ubaguzi; ni wakati muafaka wa kutakasa vitendo vyote vinavyopelekea uvunjifu wa haki msingi za binadamu zinazohatarisha afya ya familia nzima ya binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka katika Jumuiya ya Kwanza ya Wakristo kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Mtendo ya Mitume. Ni waamini waliojiaminisha kwenye huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Hii ni Jumuiya iliyosimikwa kwenye mihimili mikuu minne yaani: Fundisho la Mitume, Ushirika, Adhimisho ya Ekaristi Takatifu na Maisha ya Sala. Katika Jumuiya ile, Mtume Tomaso peke yake, ndiye aliyekuwa amebaki nyuma, akichechemea! Sehemu ndogo sana ya familia ya binadamu inaonekana kupiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini watu wengi, bado wanasuasua. Hii ni changamoto kwa kila mtu kujifunga kibwebwe ili kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kama anavyosema Mtakatifu Maria Faustina Kowalska: waamini wajitahidi kumwona Kristo anayeteseka kati ya jirani zao na wala kamwe wasionekane kama wategemezi. Ni wakati wa kunafsisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu. Watu wawe na huruma na upendo hata kama kuna wakati huruma na upendo hautendewi haki. Ustawi, mafao na ustawi wa wengi, kiwe ni kipaumbele cha kwanza kwa kila mtu!

Dominika ya Huruma ya Mungu

 

07 April 2024, 14:32

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >