Waamini Tangazeni na Kushuhudia Imani Yenu kwa Kristo Mfufuka
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, imani ni fadhila ya kimungu ambayo inamwezesha mwamini kumsadiki Mungu na kila anachosema na alichowafunulia, na ambacho Kanisa Takatifu linawataka kukisadiki, kwa sababu Yeye ndiye ukweli wenyewe. Kwa imani mwanadamu hujitoa nafsi yake yote kwa Mungu. Ni kwa sababu hiyo mwamini hutafuta kujua na kufanya mapenzi ya Mungu. Mwenye haki ataishi kwa imani na imani hai hutenda kazi kwa upendo. Paji la imani linadumu ndani yake ambaye hakutenda dhambi dhidi yake: lakini imani bila matendo imekufa. Imani ikinyimwa matumaini na mapendo haiwezi kumwunganisha kikamilifu na Kristo Yesu, na hawezi kuwa kiungo hai cha mwili wake. Mfuasi wa Kristo anapaswa kuiungama, kuishuhudia kwa uhakika na kuineza, tayari hata kufuata ile Njia ya Msalaba na madhulumu. Huduma na ushuhuda wa imani ni vya lazima kwa wokovu: “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele ya Baba aliye mbinguni. Lakini yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.” Mt 10: 32-33. Rej. KKK 1814 – 1815. Injili ya Dominika ya tatu ya Kipindi cha Pasaka Mwaka B wa Kanisa inamwonesha jinsi Kristo Mfufuka alivyowatokea wafuasi wa Emau, akaambatana nao njiani, akawafafanulia Maandiko Matakatifu na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate. Wale wafuasi walikuwa wanawashirikisha Mitume wa Yesu ile furaha ya ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu. Wakati wakisimulia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, Kristo Mfufuka akawatokea. Hii inaonesha umuhimu wa kushirikishana zawadi ya imani katika maisha.
Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 14 Aprili 2024 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, leo hii kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, kuna uwezekano mkubwa wa kupokea taarifa nyingi, ambazo baadhi yao ziko juu juu tu, nyingine zinaonesha udadisi na nyingine nyingi ni zile ambazo “si mali kitu.” Kuna habari ambazo zinasababisha huzuni, mateso na mahangaiko kwa binadamu. Lakini pia kuna habari njema na kwamba, hizi ndizo zile habari ambazo watu wanapaswa kushirikishana; katika ukweli wake: kwa kuzingatia mazuri au ubaya wake; hizi ni habari zinazogusa “sakafu ya maisha ya mwanadamu, na msaada mkubwa kwa wengine. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi, kusimulia habari za kukutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao, bila ya “kujidai” kuwa ni mwalimu, bali kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yao kwamba, Kristo Yesu yu hai na kuwa yuko karibu sana na waja wake. Huyu ndiye Kristo Yesu mfufuka anayewasha nyoyo za watu kwa furaha, na yuko tayari kuwapangusa machozi yao na hivyo kuwakirimia faraja, imani na matumaini; nguvu, ari, mwamko mpya pamoja na msamaha wa dhambi zao; huruma na amani ya kudumu. Hii ni habari njema, ambayo Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba wanaishirikisha ndani ya familia zao, katika jumuiya ya waamini wanaowazunguka pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.
Huu ni mwaliko pia wakuzungumza na kushirikishana mambo mazuri katika maisha kwani yanaongoza na kuratibu mwenendo mzima wa maisha pale walipojiweka wazi mbele ya Mungu. Bila kusahau magumu wanayokabiliana nayo, ili kuyafahamu na hatimaye, kusonga mbele katika imani kwa ari na moyo mkuu. Baba Mtakatifu anawaambia waamini kwamba, ikiwa kama mambo haya watamshirikisha Kristo Yesu, kama ilivyotokea kwa Mitume wake na hivyo waweze kuboresha mikutano na mazingira yao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, kujaribu kukumbuka tukio muhimu sana katika maisha yao ya imani, siku ile walipokutana na Kristo Yesu katika maisha! Waamini wajiulize, Je, wamewahi kuwashirikisha jirani zao tukuio hili? Je, wameligeuza tukio hili kuwa ni zawadi kwa ndugu, jamaa na marafiki; wanajumuiya au kwa watu wao wapendwa na wale wa karibu. Je, watu hawa walivutwa na tukio hili; Je, waamini wanajitahidi kujenga utamaduni wa kuwasilikiza wengine wanapowasimulia kuhusu mkutano wao na Kristo Yesu? Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumkimbilia Bikira Maria kwa sala, ili awasaidie kuwashirikisha wengine imani, kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya jumuiya zao, ili kwa hakika ziweze kuwa ni mahali muafaka pa kukutana na Kristo Yesu Mfufuka.