Mtakatifu Petro Amekabidhiwa Ufunguo wa Ufalme wa Mbinguni: Uongozi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, tarehe 29 Juni 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kubariki Pallia takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 42 na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi zao kwa wakati muafaka. Baadaye, Baba Mtakatifu ameongoza tafakari ya Neno la Mungu, Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu amekazia maana ya funguo kama kielelezo cha utume wa uongozi ambao Mtakatifu Petro amekabidhiwa na Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa zima, ili kuhakikisha kwamba, anawasaidia watu wote kuona njia ya kuingia katika mlango wa Kanisa na kuendelea kuwa mwaminifu kwa tunu msingi za Injili hadi mauti! Mtakatifu Petro alikabidhiwa funguo kwa sababu ya unyenyekevu na uaminifu wake, akajiaminisha chini ya huruma na upendo wa Mungu.
“Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za Ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani; litakuwalimefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Mt 16:19. Ufunguo ni alama ya Ufalme wa Mungu unaofanana na Punje ya haradali, Chachu, Hazina na Lulu yenye thamani kubwa. Ufalme wa Mungu umefanana kama juya, unaoweza kufikiwa kwa kujikita katika fadhila ya uvumilivu, umakini, udumifu na unyenyekevu. Kumbe, dhamana na utume ambao Kristo Yesu amemkabidhi Mtakatifu Petro ni kuwasaidia watu wote waweze kuona njia na hatimaye kuingia katika Ufalme wa Mungu, wakiwa waaminifu kwa tunu msingi za Injili ya Kristo Yesu.
Mtakatifu Petro alijitahidi kuwa mwaminifu katika maisha yake yote, kiasi hata cha kuyamimisha kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni Mtakatifu aliyeteleza, akaanguka na kusimama, kiasi hata cha kugundua ndani mwake ile furaha na uhuru unaobubujika baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Mtakatifu Petro alitubu na kumwongokea Mungu na akawa na ujasiri wa kufungua Lango la maisha yake kwa Kristo Yesu. Hata baada ya kuungama kwamba, Kristo Yesu alikuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai, bado aliteleza na kuanguka, kwa kukataa kukubali Unabii juu ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Rej. Mt 16:21-23. Mtakatifu Petro alikabidhiwa ufunguo si kwa sababu alikuwa mkamilifu, lakini ni kwa sababu alikuwa mnyenyekevu na mwaminifu, kiasi cha kupewa zawadi ya imani, kuwa ni kinga yake. Katika maisha na utume wake, Mtakatifu Petro akajiaminisha chini ya huruma na upendo wa Mungu na akabahatika kupata nguvu ya kuweza kuwaimarisha hata ndugu zake katika imani. Rej. Lk 22:32.
Baba Mtakatifu anawauliza waamini swali la msingi ikiwa kama wanayo hamu na shauku ya kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa njia ya neema ya Mungu; kwa msaada wake, wanaweza kuwa walinzi na wakarimu kwa jirani zao. Je, kwa kufanya yote haya, wanajiweka chini ya uongozi wa Kristo Yesu na Roho Mtakatifu anaye ishi ndani mwao? Bikira Maria Malkia wa Mitume na Watakatifu Petro na Paulo Mitume wawasaidie waamini kwa sala na maombezi yao ili kila mwamini aweze kujisadaka kwa ajili ya jirani zake ili kuwa ni mlinzi na kiongozi atakayewawezesha kukutana na Kristo Yesu.