Ushuhuda wa Maisha ya Hadhara ya Kristo Yesu: Uhuru Kamili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 10 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, hususan Injili kama ilivyoandikwa na Marko 3: 20-35 inamwonesha Kristo Yesu akizungumzia kuhusu shutuma kwamba, alikuwa anatoa Shetani kwa mkono wa Beelzebuli na kwamba, kwa yeyote anaye kufuru dhidi ya Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele. Kwa vile walivyosema, ana pepo mchafu. Ni katika muktadha huu wakaja mamaye na nduguze; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita, lakini Kristo Yesu akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, “Tazama, mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana mtu yeyote atakayefanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.” Hizi zote zilikuwa ni hofu za ndugu zake na viongozi, lakini Kristo Yesu alikuwa anatangaza Habari Njema ya Wokovu na kuwaponya wagonjwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtakatifu aliyekuwa anamfanya kuwa huru, yaani alimkirimia uwezo wa kupenda na kuhudumia bila kufungwa na makandokando yake.
Uhuru wa Kristo Yesu ndicho kiini cha tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 9 Juni 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kristo Yesu alikuwa huru dhidi ya mali za ulimwengu; alikuwa huru dhidi ya uchu wa madaraka na wala hakutafuta umaarufu wowote, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa watu huru dhidi uchu wa mali, madaraka na umaarufu, kwani kwa kujifungamanisha na mambo haya, waamini wanageuka na kuwa watu wake. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu alikuwa huru na wala hakutaka mali za dunia hii zimfunge, ndiyo maana akaamua kuondoka mjini Nazareti, ili kuzama katika njia ya umaskini, huku akiwaganga na kuwatibu wagonjwa; akasikiliza shida na mahangaiko ya watu mbalimbali na kuwajibu kikamilifu na wala hakuomba chochote kutoka kwao. Rej. Mt 6:25-34; Mt 10:8.
Kristo Yesu hakuwa na uchu wa madaraka; daima alitoa mwaliko kwa watu kumfuasa, lakini kamwe hakumlazimisha mtu awaye yote amfuate; wala hakuunga mkono hoja za watawala, daima alijitambulisha na kujiona kati ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; na hivyo akwafundisha wafuasi wake, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini. Rej. Lk 22: 25-27. Kristo Yesu alikuwa huru na wala hakujihusisha kutafuta umaarufu, ndiyo maana daima akajikita kutangaza na kushuhudia ukweli, hata kama hakueleweka na watu wa nyakati zake. Rej. Mt 3:21. Alisimamia ukweli hata akateswa na kufa Msalabani na wala hakuwaachia watesi wake nafasi ya kumjengea hofu, wala kumnunua na kwamba wafuasi wake walipaswa kuwaogopa wale wanaoweza kuangamiza mwili na roho. Rej. Mt 10: 28. Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kuhakikisha kwamba, hata wao wanakuwa watu huru na wala wasimezwe na malimwengu kwa kuwa na uchu wa mali na madaraka; kwa kutafuta umaarufu, kwani matokeo yake watageuka na kuwa ni watumwa wa mambo haya.
Huu ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu kuchuchumilia na kuambata upendo wa Mungu unaosheheni nyoyoni mwa waja wake; upendo wanaopaswa kuwashirikisha wengine bila hofu wala masharti, ili hatimaye, waweze kukua na kukomaa katika uhuru, kwa kueneza harufu nzuri ya uhuru kwa wale wanaowazunguka, katika familia na katika jumuiya zao. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiuliza ikiwa kama wako huru? Au wamekuwa ni wafungwa na mateka wa uchu wa mali na madaraka, kiasi cha kusadaka amani na utulivu wa ndani. Je, katika uhalisia wa maisha, Wakristo wamekuwa ni mfano bora ya kuigwa na wengine, au wamekuwa ni wafungwa wa fedha na mali, madaraka na mafaniko ya maisha, kiasi cha kusadaka amani na utulivu wa ndani. Je, waamini wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa kutangaza na kushuhudia uhuru, ukweli, sadaka na majitoleo katika familia, maeneo ya kazi. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie waamini kuishi na kupenda kama alivyopenda na kuwafundisha wafuasi wake; yaani uhuru wa wana wa Mungu. Rej. Rum 8:15 na 15; 20-23.