Kristo Yesu Ni Chakula Kinachozima Njaa na Kiu ya Maisha ya Uzima wa Milele

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 4 Agosti 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Anasema, watu waliolishwa kwa mikate mitano na samaki wawili walikuwa ni wadau wakuu walioshuhudia mang’amuzi ya msingi katika hija ya maisha yao ya kiroho, lakini wakaambulia kuona mikate mitano na samaki wawili; chakula cha kimwili, kisichoweza kuzima njaa na kiu ya maisha ya uzima wa milele. Yesu ni mkate wa uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 18 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, Kristo Yesu anapenda kuwaalika wafuasi wake kutambua kwamba, Yeye, ndio ule Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, unaozima njaa na kiu ya maisha ya uzima wa milele. Wayahudi walionja pia ukarimu wa Mwenyezi Mungu wakati walipokuwa Jangwani alipowapatia mana iliyoshuka kutoka mbinguni waliyokula wakashiba wakati wote wa safari yao hadi pale walipofika kwenye nchi ya ahadi. Yesu anawahakikishia wafuasi wake kwamba, Yeye ndiye ule Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, unaomkirimia mwamini maisha ya uzima wa milele, kwani Yeye ni Mwana mpendwa wa Mungu, aliyekuja hapa duniani kumkirimia mwanadamu utimilifu wa maisha yake na hatimaye, kumwingiza katika maisha ya Kimungu. Waisraeli walitambua kwamba, wao walishibishwa kwa namna ya pekee na: Sheria pamoja na Neno la Mungu; mambo ambayo yaliwatofautisha Waisraeli na Makabila mengine, kwani wao walikuwa na uwezo wa kutambua utashi wa Mungu na hivyo walipaswa kuwa na dira makini kuhusu maisha yao.

Kristo Yesu ni mkate wa maisha ya uzima wa milele
Kristo Yesu ni mkate wa maisha ya uzima wa milele

Kristo Yesu ni Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutekeleza mapenzi ya Mungu maishani mwao. Kitendo cha Wayahudi kupinga kuhusu Yesu kuwa ni Chakula cha uzima wa milele ni ushahidi tosha kabisa wa kupinga kazi ya Mungu. Ndiyo maana wanajikwaa kwake, kwani walishindwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na hivyo wakakosa ile fursa ya kumpokea kama Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Mioyo ya Wayahudi hawa ilikuwa mbali sana na Mwenyezi Mungu, hawakusikia hata mara moja ile kiu na njaa, kwa sababu walikuwa ni wagonjwa wa maisha ya Kiroho. Mkate unaotolewa na Kristo Yesu Neno wa Mungu, unahitaji: kiu na njaa ya undani wa maisha ya binadamu. Huu ni mwaliko wa kujiuliza ikiwa kama waamini wana njaa na kiu ya kweli ya Neno la Mungu pamoja na kufahamu maana halisi ya maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kujiachilia mikononi mwa Kristo mwenyewe, ili aweze kuwafundisha namna ya kumwamini, kukutana na hatimaye, kulishwa naye, ili kufanikisha jitihada za kupata maisha ya kweli na njia inayoelekeza maana ya maisha, haki, ukweli na upendo. Ni changamoto kwa waamini kumwamini Kristo Yesu, ili waweze kupata maisha mapya.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano

Ni katika muktadha wa muujiza wa Kristo Yesu kuulisha umati mkubwa wa watu kwa mikate mitano na samaki wawili na umuhimu wa kushirikishana na wengine hata kile kidogo kilichopo, watu wote wanaweza kutosheka kwa wema na ukarimu wa Mungu. Lakini, Wayahudi hawakuelewa maana ya muujiza na ishara ile aliyotenda Kristo Yesu, wakadhani kwamba, kile kilikuwa ni “kiini macho” ndiyo maana wakaanza kumtafuta tena. Rej Yn 6:24-35. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 4 Agosti 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, watu hawa walikuwa ni wadau wakuu walioshuhudia mang’amuzi ya msingi katika hija ya maisha yao ya kiroho, lakini wakaambulia kuona mikate mitano na samaki wawili; chakula cha kimwili, kisichoweza kuzima njaa na kiu ya maisha ya uzima wa milele. Mkate waliopewa Wayahudi, ilikuwa ni alama iliyokuwa inawaelekeza kwenye maisha ya uzima wa milele.

Kristo Yesu ni chakula cha uzima wa milele
Kristo Yesu ni chakula cha uzima wa milele

“Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.” Yn 6:35. Kristo Yesu ndio ule Mkate wa uzima wa milele, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kuja kushirikiana na binadamu katika umaskini wake, ili kumwongoza, aweze kufikia furaha ya kweli katika ushirika mkamilifu na Mwenyezi Mungu, kwa njia ya zawadi na sadaka ya maisha yake. Rej Yn 3:16. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema ni upendo peke yake unaoweza kumpatia mwanadamu utimilifu wa maisha; ndio upendo ambao unapaswa kushirikishwa kwa wengine. Hayo ndiyo yanayoendelea kujiri ndani ya familia, inayojibidiisha kuhakikisha kwamba, watoto wanakuwa na uhakika wa maisha kwa siku za mbeleni. Na watoto wanapaswa kuonesha upendo huu kwa kushirikiana na ndugu zao. Lakini inasikitisha kuona watoto wakipigania urithi kutoka kwa wazazi wao, kiasi cha kushindwa hata kuzungumza kati yao. Watoto wakumbuke kwamba, ujumbe mahususi wanaowaachia wazazi wao ni ule upendo wa dhati na wala si fedha na mali, kama ambavyo anafanya pia Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Jambo la msingi ni waamini kujiuliza ni uhusiano gani ambao wamejenga na mambo ya ulimwengu huu? Je, haya mambo yamewageuza na kuwa ni watumwa? Au ni watu huru, vyombo na mashuhuda wa kupokea na kutoa upendo! Je, waamini wamejenga utamaduni wa kumshukuru Mungu na jirani zao, kwa zawadi na karama walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, tayari kuwashirikisha wengine kwa furaha? Bikira Maria aliyesadaka maisha yake yote kwa Kristo Yesu, awafundishe kutenda mambo yote kama vyombo na mashuhuda wa upendo.

Yesu Mkate wa Uzima

 

04 August 2024, 15:17

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >