Tafuta

Mwili na Damu Azizi ya Yesu: Chakula Kilichoshuka Kutoka Mbinguni: Fundisho Gumu

“Bwana! twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.” Yn 6: 68-69. Hili ni jibu linaloshuhudia urafiki kati ya Yesu na Mitume wake; imani thabiti inayowaunganisha. Na Mtakatifu Petro, Mtume anatoa jibu katika hali tete, baada ya Kristo Yesu kutoa katekesi ya kina kuhusu: Mwili na Damu yake Azizi; Chakula kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya maisha na uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu akasema, “Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.  Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.” Yn 6:65-69. Hii ni sehemu ya Injili ya Yohane inayobeba mafundisho mazito kutoka kwa Kristo Yesu juu ya umuhimu wa kula Mwili wake na kuinywa Damu yake Azizi, kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele. Na hapa Mtakatifu Petro Mtume anatoa jibu mujarabu linayokita mizizi yake katika imani na matumaini “Bwana! twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.” Yn 6: 68-69. Hili ni jibu linaloshuhudia urafiki kati ya Kristo Yesu na Mitume wake; imani thabiti inayowaunganisha: Mitume na wafuasi wengine kwa Kristo Yesu. Mtakatifu Petro anatoa jibu katika hali tete, baada ya Kristo Yesu kutoa katekesi ya kina kuhusu: Mwili na Damu yake Azizi; Chakula kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya maisha na uzima wa milele. Hii ilikuwa ni lugha ngumu kuweza kueleweka mara moja na wafuasi wake, hata na Mitume wake, kiasi cha wanafunzi wake wengi kurejea nyuma na kushindwa kuandamana naye. Lakini wale thenashara, wakabaki wamesimama imara katika imani, kwa sababu katika Kristo Yesu walipata maneno ya uzima wa milele. Wamemsikia, akiwafundisha watu wa Mataifa, akihubiri; akiganga na kuwaponya watu magonjwa yao ya kiroho na kimwili; wakashuhudia akitenda miujiza pamoja na kushiriki naye kwa undani zaidi katika maisha ya hadhara. Rej. 3:7-19.

Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani
Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani

Haikuwa rahisi na wala hata sasa si rahisi kutambua yale yaliyokuwa yakitendwa na Kristo Yesu, kiasi kwamba, inawawia vigumu wafuasi wake kuupokea upendo wake, changamoto za huruma ya Mungu; maisha ya kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza. Rej. Mt 18:21-22. Vipaumbele vya Kristo Yesu, wakati mwingine vilikuwa vinatofautiana na baadhi ya misimamo ya kidini na hata mapokeo, kiasi cha kuwachukiza wengi. Rej. Mt 15:12. Si rahisi kumfuasa Kristo Yesu. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, Dominika tarehe 25 Agosti 2024. Baba Mtakatifu anakaza kusema, pamoja na waalimu wa dini wa nyakati zao, hawakuweza kufanikiwa kumpata jaalimu makini aliyezima kiu na njaa ya maisha yao ya kiroho kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, chemchemi ya furaha ya kweli, upendo wa dhati na kwamba, ni katika Kristo Yesu, wanaweza kupata utimilifu wa maisha, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu, dhambi na kifo. Mitume wa Yesu licha ya mapungufu yao ya kibinadamu, toba na wongofu wa ndani, waliweza kudumu na kubaki na Kristo Yesu mpaka siku ya mwisho, isipokuwa yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. Rej. Yn 17:12.

Bwana twende kwa nani, Wewe una maneno ya uzima wa milele.
Bwana twende kwa nani, Wewe una maneno ya uzima wa milele.

Hali ya kumkataa Kristo Yesu na mafundisho yake, inawakumba na kuwaandama hata Wakristo katika ulimwengu mamboleo anasema Baba Mtakatifu Francisko. Si rahisi sana kumfuasa Kristo Yesu na kutenda kama anavyotaka, kwa kuzingatia vigezo, vipaumbele sanjari na mifano yake. Kadiri ya jinsi ambavyo waamini wanamkaribia Kristo Yesu, ndivyo hivyo wanaweza kumwilisha ndani mwao tunu msingi za Injili; kwa kupokea neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa; katika maisha ya sala inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu na kumwilishwa katika Injili ya upendo. Kwa kufanya hivi, waamini wataweza kukutana na Kristo Yesu kama rafiki na mwandani mwa safari, ili hatimaye, kuambanatana naye kama “Neno la uzima.” Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya upembuzi yakinifu katika maisha yao, ili kuangalia uwepo wa Kristo Yesu katika maisha yao; kwa jinsi gani wanavyomwachia Kristo Yesu nafasi ya kugusa, kuganga na kuwaponya kutoka katika undani mwao, yeye ambaye ni “Neno la uzima.” Bikira Maria alimpokea Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, ili awasaidie waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kumsikiliza Kristo Yesu sanjari na kuambatana naye katika safari ya maisha yao, huku Bondeni kwenye machozi, bila kumgeuzia kisogo hata mara moja!

Mafundisho ya Yesu

 

25 August 2024, 14:13

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >