Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho: Furaha na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, Mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe, kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos.” Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae.”
Hii ni Sherehe inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila Mwaka ifikapo tarehe 15 Agosti. Mwili wa Bikira Maria uliokuwa umekingwa na dhambi ya asili, ukapalizwa mbinguni. Hiki ni kielelezo makini cha imani ya watu wa Mungu kama alivyokiri Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2024 anasema, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumtafakari Bikira Maria baada ya kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu aliondoka, akaenda hata nchi ya mlimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti, binamu yake! Rej Lk 1: 39-56. Taarifa kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, ili msukuma kuondoka kwa haraka, ili kwenda kutangaza na kushuhudia ile furaha iliyomwilishwa katika huduma. Tangu wakati huo, Bikira Maria alianzisha mchakato wa kumfuasa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu, kama mfuasi halisi wa Ufalme wa Mungu, akadiriki hata kusimama chini ya Msalaba na hatima ya hija hii ya maisha ya kiroho ni Kupalizwa kwake mbinguni, ambako huko juu mbinguni wanaendelea kufurahia pamoja na Kristo Yesu, maisha ya uzima wa milele. Bikira Maria ni mfano wa mwamini anayesoma alama za nyakati, akawa tayari kufuata nyayo za Mwanaye mpendwa, akakutana na wafuasi wa Kristo Yesu na baadaye safari yake ya kutangulia kwenda mbinguni, kwenye utukufu wa Baba wa milele.
Huu ni mwaliko kwa waamini kutambua kwamba, maisha yao huku bondeni kwenye machozi ni safari endelevu itakayofikia hatima yake kwa kukutana na Kristo Yesu, huko mbinguni. Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanatunza nyoyoni mwao, kwamba, Mwenyezi Mungu amewaumba, ili hatimaye, waweze kuwa na furaha ya uzima wa milele na kwamba, ndoto yake ni kuwachukua waja wake wote, ili wakaishi naye katika maisha ya uzima wa milele. Safari ya maisha ya binadamu ni sehemu ya mpango wa upendo wa Mungu kwa binadamu, hii ni hija inayowaongoza siku hadi siku, ili kukutana na Mwenyezi Mungu, chemchemi ya furaha isiyokuwa na mwisho; furaha ambayo amewaandalia waja wake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanarutubisha safari hii kwa matumaini na hasa pale, wanapokumbana na magumu pamoja na changamoto za maisha. Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, iwe ni fursa makini kwa waamini kujiuliza swali la msingi, ikiwa kama katika safari ya maisha yao hadi duniani, wanaendelea kuirutubisha kwa matumaini, kwa kutambua kwamba, mwisho wa safari yao, yuko Kristo Yesu anayewangoja. Au katika safari hii ya maisha, tayari wamekwisha “kubweteka?” Je, waamini wanakumbuka kwamba, wameumbwa kwa ajili ya kufurahia maisha ya uzima wa milele; kwa kuwapenda na kuwathamini ndugu na jirani au mwamini amejikuta akiwa amezama zaidi katika uchoyo na ubinafsi na hatimaye, kuzama katika malimwengu? Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwangalia na hatimaye, kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwaombea, ili kamwe wasisahau kwamba, hatima ya maisha yao ni furaha na matumaini ya uzima wa milele. “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo.” Efe 1:18.
Wakati huo huo, Kardinali Pierbattista Pizzaballa, O.F.M. Patriaki wa Yerusalemu na Mlinzi mkuu wa Nchi Takatifu na Mlima wa Sion, katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, yaliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mateso lililoko kwenye Mlima wa Mizeituni ulioko Mashariki mwa mji wa Yerusalemu. Ametumia fursa hii kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati. Katika mahubiri yake amewaalika waamini kumtafakari Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho kama zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, changamoto kwa walimwenguni ni kuondokana: vita, ghasia, machafuko; Utumwa mamboleo na biashara ya ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu pamoja na ukoloni mamboleo. Bikira Maria, Mama wa Yesu akiwa amekwisha kutukuzwa mbinguni mwili na roho, ni sura na mwanzo wa Kanisa ambalo litapata utimilifu wake katika ulimwengu ujao. Kadhalika anang’aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na ya faraja kwa taifa la Mungu lililo safarini, mpaka siku ya Bwana itakapokuja. LG 68. Amezungumzia kuhusu madhara ya vita, yanayowatumbukiza watu katika umaskini wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, kwa kusigina, uhuru, utu, heshima na haki zao msingi. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni, awaombee walimwengu haki, amani na upatanisho.