Nicaragua,maaskofu Álvarez na Mora na mapadre wengine waachiliwa.Wamekaribishwa Vatican
Vatican News
Askofu Rolando Álvarez, aliyekamatwa kwa zaidi ya mwaka mmoja, Askofu Isidoro del Carmen Mora Ortega, waseminari wawili, mapadre kumi na watano. Kwa jumla, wawakilishi 19 wa Kanisa Katoliki la Nicaragua waliachiliwa huru na serikali ya Nicaragua. Habari hiyo, iliyoenezwa na vyombo vya habari vya ndani, ilithibitishwa na serikali ya Managua. Isipokuwa mmoja aliyebaki Venezuela, wote walifika mjini Roma na sasa ni wageni wa Vatican. Askofu Álvarez, wa Matagalpa na msimamizi wa kitume wa Jimbo la Estelí, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 26 jela, alikuwa gerezani tangu Februari mwaka 2023 baada ya kuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu Agosti 2022. Wakati Askofu Mora alikamatwa mnamo Desemba 2023.
Katika sala ya Malaika wa Bwana mwanzoni mwa mwaka, akikumbuka hali ya maaskofu na mapadre "kunyimwa uhuru" katika nchi ya Amerika ya Kati, Papa Francisko alihakikishia "ukaribu wake katika sala", huku akiwaalika watu wa Mungu kuiombea nchi ya Nicaragua, kwa ajili ya amani na alielezea matumaini "kwamba sisi daima tunatafuta njia ya mazungumzo ili kuondokana na matatizo".
Tayari mnamo Oktoba, 2023 mapadre 12 wa Nicaragua waliachiliwa kutoka gerezani. Vatican ilikuwa imekubali ombi la kuwapokea. Kwa njia hiyo wamekaribishwa jijini Roma, katika baadhi ya majengo ya Jimbo la Roma.