Tafuta

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Unyenyekevu

Liturujia ya Neno la Mungu inawapeleka waamini hadi nyumbani kwa B. Maria mjini Nazareti anaposalimiwa na Malaika Gabrieli akisema salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Ni katika mazingira ya kifamilia, Mwenyezi Mungu anawafunulia waja wake uzuri wa Moyo Safi wa Bikira Maria, aliyejaa neema, yaani asiyekuwa na doa la dhambi, kwani amekingiwa dhambi ya asili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba mwaka 1854 katika Waraka wake wa Kitume “Ineffabilis Deus”, alitangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria! Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Desemba. Sherehe haitukuzi tu usafi, uzuri na utakatifu wa Bikira Maria bali ni fundisho la imani ambalo waamini wanapaswa kuliamini kina. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jumatano tarehe 8 Desemba 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbusha waamini kwamba, Liturujia ya Neno la Mungu inawapeleka watu wa Mungu hadi nyumbani kwa Bikira Maria mjini Nazareti anaposalimiwa na Malaika Gabrieli akisema salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Rej. Lk 1: 26-38. Ni katika mazingira ya kifamilia nyumbani, Mwenyezi Mungu anawafunulia waja wake uzuri wa Moyo Safi wa Bikira Maria, aliyejaa neema, yaani asiyekuwa na doa la dhambi, kwani amekingiwa dhambi ya asili.

Lakini kwa salamu hii, Bikira Maria, alishangaa na kufadhaika sana kwa sababu alipokea Salamu iliyosheheni sifa kubwa, jambo ambalo lingeweza kumjengea “majigambo na kiburi.” Kristo Yesu anawatahadharisha wanafunzi wake wasipende kuvaa mavazi marefu, kusalimiwa masokoni na kuketi katika Masinagogi na viti vya mbele karamuni. Kwa maneno machache wasipende kujikuza bali wajitahidi kuwa wapole na wanyenyekevu wa moyo. Bikira Maria kwa kusikia salamu hii, akafadhaika sana na kushangaa na wala hakujikweza. Anausikia uzito wa salamu na kujisikia mdogo sana ndani mwake mbele ya Mwenyezi Mungu. Unyenyekevu wa Bikira Maria ni kivutio kikubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Ni katika mazingira ya familia nyumbani, Bikira Maria anapokea sifa ambazo hakuwahi hata siku moja kujipatia mwenyewe na kuyapokea yote haya kwa moyo wa unyenyekevu pasi na makuu, kwa kutambua kwamba, yale yote aliyokirimiwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Uhuru binafsi wa Bikira Maria anausadaka kwa ajili ya Mungu na mafao ya wengine. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili amejaliwa macho kwa ajili ya Mungu pamoja na jirani zake. Fadhila ya unyenyekevu inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwenye kuta za familia na katika hali ya kificho na wala si katika maeneo ya wazi au kwenye barabara kuu za mji wa Nazareti. Hii ndiyo habari kuu kwa waamini wote kwamba, Mwenyezi Mungu anatenda miujiza na mambo makuu kwa watu wanyenyekevu, wanaotoa kipaumbele kwa Mungu na jirani zao.

Ni katika kuta za nyumba ndogo ya Bikira Maria, Mwenyezi Mungu ametenda makuu na kubadili historia ya mwanadamu. Hata leo hii, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mwenyezi Mungu anapenda kutenda maajabu pamoja na watu wake, ili kuleta mabadiliko katika: familia, maeneo ya kazi na katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu, mahali ambapo neema na baraka ya Mungu inatenda kazi. Baba Mtakatifu anawauliza waamini swali msingi, Je, wanaamini juu ya utakatifu wa maisha, au wanadhani kwamba, ni jambo la kufikirika tu; au ni kwa ajili ya wafanyakazi peke yao, au ndoto ya mchana ambayo haina uhalisia katika maisha ya kila siku? Baba Mtakatifu amehitimisha tafakari yake kuhusu Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kwa kuwaalika waamini kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwaombea neema na baraka ya kutambua utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Wajitahidi kuishi kila kukicha kwa kujikita katika unyenyekevu, huku wakiwa ni watu wenye furaha. Kama watu binafsi wajitahidi kuwa huru, huku macho yao yakiwa yanamwelekea Mwenyezi Mungu na jirani wanaokutana nao katika hija ya maisha. Waamini wawe na ujasiri kwani wamepewa “kitambaa cha kushonea” utakatifu wa maisha. Pale wanaoshindwa na kuanza kukata tamaa, wamkimbilie Bikira Maria, ili aweze kuwaangalia kwa macho yenye huruma, kwani hakuna mtu aliyekimbilia ulinzi na tunza yake, hasimsikileze kamwe.

Papa Bikira Maria
08 December 2021, 15:40

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >