Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Mshangao na Uaminifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Bikira Maria alipata upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyemkirimia karama na neema nyingi ili aweze kuwa ni Mama wa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Karne kwa karne Mama Kanisa ametambua kwamba, Bikira Maria aliyejazwa neema na Mwenyezi Mungu, alikombolewa tangu mwanzo alipotungwa mimba! Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria! “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.” Lk 1:26-38.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili tarehe 8 Desemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amekita tafakari yake kuhusiana na “Mshangao wa Bikira Maria kwa matendo makuu ya Mungu na Uaminifu katika mambo ya kawaida.” Mshangao wa Bikira Maria kwa matendo makuu ya Mungu katika maisha yake unatokana na maneno ya Malaika Gabrieli “Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?” Anashangaa kuambiwa kwamba, amejaa neema yaani upendo wa Mungu unafurika katika maisha yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kushangaa mbele ya zawadi, neema na baraka nyingi wanazokirimiwa na Mwenyezi mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kumbe, wanawajibika kuzithaminisha, kuzifurahia na hatimaye, kuzitolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ushuhuda unaosimikwa katika unyenyekevu licha ya matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika safari ya maisha yake hapa duniani. Jambo la msingi kwa waamini kujiuliza ni ikiwa kama wanashangazwa na matendo makuu ya Mungu katika maisha yao ya kila siku na ikiwa kama wako tayari kuwashirikisha jirani zao.
Mwelekeo wa pili anasema Baba Mtakatifu ni uaminifu katika mambo ya kawaida. Kabla ya Malaika Gabrieli kumpasha Habari Bikira Maria kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, hakuna jambo lolote lililoandikwa kumhusu Bikira Maria. Bikira Maria alikuwa ni msichana wa kawaida kama wasichana wengine wote kijijini kwake Nazareti, akabahatika kuutunza Moyo wake Mtakatifu, usiokuwa na doa, Moyo ambao kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili, ili aweze kuipokea na hatimaye kuitunza zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Bikira Maria aliweza kukuza na kudumisha Moyo Safi katika maisha ya kawaida: Kwa kusikiliza Neno la Mungu lililokuwa likisomwa kwenye Sinagogi na alifanikiwa kuhifadhi baadhi ya maneno yanayosomeka kwenye Injili; alikuwa na imani kubwa, amana na urithi mkubwa kutoka kwa wazazi wake. Na hivyo kwa njia ya maisha ya kawaida, Bikira Maria aliweza kuruhusu zawadi ya Mungu kukua ndani mwake na hivyo kujifunza kusema, “Ndiyo” kwa njia ya maisha yake yote. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu amewataka waamini kuchunguza ndani mwao, ikiwa kama katika hija ya maisha ya kiroho wamekuwa ni waaminifu mbele ya Mungu, Je, wanatafuta mwanya wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu? Je, wanasali na kushiriki kikamilifu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho? Je, wanajitahidi kutoa huduma kwa wahitaji. Haya ni matukio madogo madogo, lakini muhimu ya kumwezesha mwamini kupokea uwepo angavu wa Mungu katika maisha yake. Bikira Maria Mkingiwa Dhambia ya Asili, awasaidie waamini kushangazwa na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kujibu kwa uaminifu ukarimu, kila siku ya maisha yao.