Tafuta

Mtakatifu Petro Amekabidhiwa Ufunguo wa Ufalme wa Mbinguni: Uongozi

Katika tafakari yake, Papa amekazia maana ya funguo kama kielelezo cha utume wa uongozi ambao Mtakatifu Petro amekabidhiwa na Yesu kwa ajili ya Kanisa zima, ili kuhakikisha kwamba, anawasaidia watu wote kuona njia ya kuingia katika mlango wa Kanisa na kuendelea kuwa mwaminifu kwa tunu msingi za Injili hadi mauti! Mtakatifu Petro alikabidhiwa funguo kwa sababu ya unyenyekevu na uaminifu wake, akajiaminisha chini ya huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, tarehe 29 Juni 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kubariki Pallia takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 42 na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi zao kwa wakati muafaka. Baadaye, Baba Mtakatifu ameongoza tafakari ya Neno la Mungu, Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu amekazia maana ya funguo kama kielelezo cha utume wa uongozi ambao Mtakatifu Petro amekabidhiwa na Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa zima, ili kuhakikisha kwamba, anawasaidia watu wote kuona njia ya kuingia katika mlango wa Kanisa na kuendelea kuwa mwaminifu kwa tunu msingi za Injili hadi mauti! Mtakatifu Petro alikabidhiwa funguo kwa sababu ya unyenyekevu na uaminifu wake, akajiaminisha chini ya huruma na upendo wa Mungu.

Ufunguo ni kielelezo cha huduma ya uongozi wa Kanisa zima
Ufunguo ni kielelezo cha huduma ya uongozi wa Kanisa zima

“Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za Ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani; litakuwalimefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Mt 16:19. Ufunguo ni alama ya Ufalme wa Mungu unaofanana na Punje ya haradali, Chachu, Hazina na Lulu yenye thamani kubwa. Ufalme wa Mungu umefanana kama juya, unaoweza kufikiwa kwa kujikita katika fadhila ya uvumilivu, umakini, udumifu na unyenyekevu. Kumbe, dhamana na utume ambao Kristo Yesu amemkabidhi Mtakatifu Petro ni kuwasaidia watu wote waweze kuona njia na hatimaye kuingia katika Ufalme wa Mungu, wakiwa waaminifu kwa tunu msingi za Injili ya Kristo Yesu.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume

Mtakatifu Petro alijitahidi kuwa mwaminifu katika maisha yake yote, kiasi hata cha kuyamimisha kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni Mtakatifu aliyeteleza, akaanguka na kusimama, kiasi hata cha kugundua ndani mwake ile furaha na uhuru unaobubujika baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Mtakatifu Petro alitubu na kumwongokea Mungu na akawa na ujasiri wa kufungua Lango la maisha yake kwa Kristo Yesu. Hata baada ya kuungama kwamba, Kristo Yesu alikuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai, bado aliteleza na kuanguka, kwa kukataa kukubali Unabii juu ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Rej. Mt 16:21-23. Mtakatifu Petro alikabidhiwa ufunguo si kwa sababu alikuwa mkamilifu, lakini ni kwa sababu alikuwa mnyenyekevu na mwaminifu, kiasi cha kupewa zawadi ya imani, kuwa ni kinga yake. Katika maisha na utume wake, Mtakatifu Petro akajiaminisha chini ya huruma na upendo wa Mungu na akabahatika kupata nguvu ya kuweza kuwaimarisha hata ndugu zake katika imani. Rej. Lk 22:32.

Yesu alimkabidhi Mtakatifu Petro Ufunguo wa Ufalme wa Mbinguni
Yesu alimkabidhi Mtakatifu Petro Ufunguo wa Ufalme wa Mbinguni

Baba Mtakatifu anawauliza waamini swali la msingi ikiwa kama wanayo hamu na shauku ya kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa njia ya neema ya Mungu; kwa msaada wake, wanaweza kuwa walinzi na wakarimu kwa jirani zao. Je, kwa kufanya yote haya, wanajiweka chini ya uongozi wa Kristo Yesu na Roho Mtakatifu anaye ishi ndani mwao? Bikira Maria Malkia wa Mitume na Watakatifu Petro na Paulo Mitume wawasaidie waamini kwa sala na maombezi yao ili kila mwamini aweze kujisadaka kwa ajili ya jirani zake ili kuwa ni mlinzi na kiongozi atakayewawezesha kukutana na Kristo Yesu.

Funguo
29 June 2024, 14:04

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >