Uongozi Katika Kanisa Unasimikwa Katika Unyenyekevu na Huduma

Mawazo ya nani ni mkubwa kati yao yalisigana na vipaumbele vya Yesu ambaye alikuwa akizungumzia kuhusu sadaka ya maisha yake, lakini kumbe, Mitume walikuwa wanajadiliana kuhusu madaraka. Hii ni aibu iliyowafunga midomo, kwani kwanza kiburi kilikuwa kimewafunga nyoyo zao. Kristo Yesu anachukua nafasi kuizungumzia changamoto hii hadharani kwa kusema “Mtu anayetaka kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote.” Mk 9:35.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, Fumbo la Pasaka la Msalaba na Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu, ambayo Mitume na Kanisa baada yao, wanapaswa kuitangaza na kuishuhudia duniani. Mpango wa wokovu wa Mungu umetimilika “mara moja tu” kwa kifo cha ukombozi cha Mwana wake, Kristo Yesu. Imani inaweza kujaribu kutafuta mazingira ya kifo cha Kristo Yesu, yaliyotajwa kiaminifu na Injili na kuangazwa na chechemi nyingine za historia kusudi iweze kujua zaidi maana ya ukombozi. Rej. KKK 571-573. Mwinjili Marko katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 25 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, Mk 9:30-37 anazungumzia kuhusu hatima ya maisha ya Kristo Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; na akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka.” Mk 9:31.

Kristo Yesu ni kielelezo cha huduma katika upendo
Kristo Yesu ni kielelezo cha huduma katika upendo

Wakati Kristo Yesu akizungumzia juu ya mateso, kifo na ufufuko wake, Mitume walikuwa na mambo mengine kabisa vichwani mwao. Wanapoulizwa walishindania nini njiani? Wakanyamaza. Hiki kimya kikuu ni muhimu sana katika tafakari ya leo, kwani walikuwa wanajadiliana wao kwa wao ni nani mkubwa kati yao. Rej. 9:34. Mawazo haya yalisigana kwa kiasi kikubwa na maneno na vipaumbele vya Kristo Yesu ambaye alikuwa akizungumzia kuhusu sadaka ya maisha yake, lakini kumbe, Mitume walikuwa wanajadiliana kuhusu madaraka. Hii ni aibu iliyowafunga midomo, kwani kwanza kiburi kilikuwa kimewafunga nyoyo zao. Kristo Yesu anachukua nafasi kuizungumzia changamoto hii hadharani kwa kusema “Mtu anayetaka kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote.” Mk 9:35. Unataka kuwa mkubwa kuliko wengine wote basi jinyenyekeze, uwe mdogo na uendelee kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wengine.

Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma ya upendo
Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma ya upendo

Baba Mtakatifu anasema Kanisa linawahitaji viongozi wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza katika maisha yao kwa ajili ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Kristo kwa ndugu zake, kwa kujikita katika upendo na unyenyekevu; uvumilivu na udumifu, ili Familia ya Mungu iweze kukua, kutembea, kujenga na kumshuhudia Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Kristo Yesu anapenda kuchukua fursa hii kama kielelezo cha upyaisho ya jinsi ya Mitume wake wanavyopaswa kuishi. Kristo Yesu anakazia umuhimu wa kuwalinda, kuwatunza na kuwapokea maskini na wadogo katika huduma, kama ilivyo kwa mtoto mdogo ambaye kimsingi hana mambo mengi. Yote haya Mitume walipaswa kuyazingatia na kuyaweka katika matendo kwa kutambua kwamba, mwanadamu ana kiu ya maisha. Uchu wa mali na madaraka wakati mwingine, unawafanya watu kushindwa kuuona ukweli huu, kwamba, wanaishi kwa sababu wamepokelewa, changamoto na mwaliko ni kuwa ni wahudumu na wala si wamiliki.

Ukitaka kuwa mkubwa, jinyenyekeshe na kujisadaka kwa ajili ya huduma
Ukitaka kuwa mkubwa, jinyenyekeshe na kujisadaka kwa ajili ya huduma

Maskini na wanyonge ni kundi la kwanza la watu wanaoteseka. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna umati mkubwa wa watu wanaoteseka na kupoteza maisha kutokana na uchu wa mali na madaraka, sehemu mbalimbali za dunia. Haya ni maisha yanayokataliwa kama walivyo mkataa Kristo Yesu, akawekwa mikononi mwa watesi wake, kiasi cha kuwamba juu ya Msalaba. Injili bado ni Neno hai na chemchemi ya matumaini: Yule ambaye amekataliwa na watu, akateswa na kufa Msalabani amefufuka na ndiye Bwana! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, kujiuliza swala la msingi, Je, wanautambua Uso wa Kristo Yesu kati ya wale wadogo na maskini? Je, kama waamini wanajibidiisha kuwahudumia jirani zao kwa ukarimu na upendo? Je, wana ujasiri wa kuwashukuru wale wote wanaowahudumia kwa moyo wa upendo na ukarimu? Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali pamoja na Bikira Maria, ili waweze kufanana naye, watu huru, bila kujikweza, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma inayosimikwa kwenye unyenyekevu.  

Ukuu Katika Kanisa
22 September 2024, 14:37

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >